Wednesday, September 29, 2010

Synovate waambiwa wawahi Mahakamani

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeivaa kampuni utafiti ya Synovate kikisisitiza kuwa kina matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni hiyo ya kupata matokeo yaliyotoa ushindi wa asilimia 45 kwa chama hicho na mgombea wake wa urais, Dkt. Willibrod Slaa.

Synovate hivi karibuni ilikanusha habari kuwa haijawahi kufanya utafiti wala kuficha matokeo hayo yaliyodaiwa kuipa CCM na mgombea wake Rais Jakaya Kikwete asilimia 41, huku ikitishia kulishtaki gazeti moja liliwakariri viongozi wa CHADEMA wakieleza utafiti huo.

Akizungumzia matokeo hayo jana, Dkt. Slaa alisema "Synovate wakimbie haraka mahakamani, tunazo document (nyaraka), hata gazeti lililotishiwa kushtakiwa lisiwe na wasiwasi, huu ni wakati wa kuvunja heshima ya Synovate kitaifa na kimataifa.

"Walifanya utafiti na katika swali namba GP 06 waliuliza, 'uchaguzi ukifanyika sasa hivi nani utampigia kura kuwa rais wa Tanzania?' na majina yote yaliweka pale ya wagombea, sasa wanakanusha nini, waende haraka sana mahakamani, vinginevyo credibility (heshima) yao tutaivuruga nchi nzima na kimataifa, alisema huku akionesha nyaraka hizo kwa mbali.

Dkt. Slaa alisema katika nchi nyingine taasisi za maoni zinakuwa huru, hazipendelei chama chochote kile.



Source (Darhotwire)