Friday, July 01, 2016

Wawekezaji wazawa wana haki kuwekeza kwenye gesi, mafuta




Wawekezaji wazawa wana haki kuwekeza kwenye gesi, mafuta
Na Greyson Mwase

Serikali imesema wawekezaji wazawa wana haki ya kuwekeza kwenye sekta za mafuta na gesi ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Hayo yamesemwa na mtaalam kutoka Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Petro Marwa kwenye maonesho ya kimataifa ya sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Petro alisema kumekuwepo na dhana kuwa wawekezaji kutoka nje ya nchi wanapewa kipaumbele katika uwekezaji kwenye gesi na mafuta jambo ambalo si sahihi.

Alisema ili kuhakikisha kuwa kila mtanzania ananufaika na uwekezaji kwenye sekta za gesi na mafuta, Serikali imeweka sheria nzuri za kuwezesha watanzania kuwa sehemu ya uchumi wa gesi na mafuta.

" Kwa mfano Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 kifungu cha 218 kinaeleza ushiriki wa serikali kupitia Kampuni ya Mafuta ya Taifa (National Oil Company) na kifungu cha 219 na 220 kinaainisha ushiriki wa watanzania katika utoaji wa huduma na bidhaa kwa makampuni yaliyowekeza nchini kwenye sekta za mafuta na gesi," alisema Mhandisi Petro.

Mhandisi Petro aliendelea kusema kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha watanzania wanakuwa si watazamaji kwenye uvunaji wa rasilimali za gesi na mafuta bali wanakuwa ni washiriki kamili na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akielezea mikakati hiyo, Mhandisi Petro alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilianzisha kozi mbalimbali zinazohusu mafuta na gesi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Madini (MRI).

Aliongeza kuwa Wizara imekuwa ikiwezesha wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kupata ufadhili wa kusomea masuala ya mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mhandisi Petro alitoa wito kwa watanzania wote kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta za mafuta na gesi ili nchi iweze kutoka kwenye kundi la nchi masikini duniani na kuingia katika orodha ya nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyofafanua.
Afisa Habari, Mhandisi Yisambi Shiwa (kulia) kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) akielezea madini ya dhahabu yanavyochenjuliwa kwa mteja aliyeshika sampuni ya madini hayo kwenye banda la TMAA katika maonesho hayo.
Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Phillip Mathayo (kushoto) akielezea majukumu ya Wizara kwa mteja aliyetembelea banda hilo katika Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba (Dar es Salaam International Trade Fair) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Washiriki kutoka Kampuni ya Kuendeleza Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba (Dar es Salaam International Trade Fair) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wateja (kushoto) akitoa maoni yake kwenye banda la Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba (Dar es Salaam International Trade Fair) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Washiriki kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba (Dar es Salaam International Trade Fair) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Neema Mwambenja kutoka Taasisi ya Environmental Foundation for Tanzania (EFFORT) ambayo ni mdau wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) (katikati) akitoa maelezo ya shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo kwenye banda la REA, kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba (Dar es Salaam International Trade Fair) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Odriana Magige kutoka taasisi hiyo.
Mhandisi Migodi kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Suleiman Khalid (katikati) akielezea shughuli zinazofanywa na shirika hilo. Kushoto ni Afisa Usalama na Mazingira kutoka shirika hilo Paul Thobias.
Banda la Wizara ya Nishati na Madini na Tasisi zake kama linavyoonekana pichani kwenye kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba (Dar es Salaam International Trade Fair) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Afisa Habari, Mhandisi Yisambi Shiwa (kushoto) na Mkaguzi wa Madini Mwandamizi Jeremiah Hango (kulia) kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA), wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kuwahudumia wateja katika Maonesho ya Kimataifa ya Saba Saba (Dar es Salaam International Trade Fair) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.