Mtalii kutoka nchini Ujerumani amefariki dunia baada ya kuanguka akijipiga picha nchini Peru.
Oliver Park, 51, alianguka kwenye eneo la mabaki ya kale ya Machu Picchu katika milima ya Andes nchini Peru.
Park alipuuza tahadhari za kiusalama na onyo kutoka kwa walinzi na akaenda eneo lisiloruhusiwa watu kujipiga picha.
Taarifa zinasema alienda kujipiga picha eneo la mwamba Jumatano.
Alijaribu kuruka juu ndipo ajipiga picha akiwa hewani lakini akateleza na kutumbukia kwenye bonde.
Maafisa wa uokoaji waliupata mwili wake Alhamisi na kuupeleka kituo cha polisi kilichoko karibu.
Polisi wamesema mwili wake utapelekwa chumba cha kuhifadhia maiti katika mji wa Cusco.