Monday, May 23, 2016

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete: BRN Iliniwezesha Kuongeza Ufanisi, Uwajibikaji na Matokeo Katika Utekelezaji wa Miradi ya Serikali



Rais Mstaafu Jakaya Kikwete: BRN Iliniwezesha Kuongeza Ufanisi, Uwajibikaji na Matokeo Katika Utekelezaji wa Miradi ya Serikali
Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshiriki katika Mkutano wa Masuala ya Afya wa Mawaziri unaoandaliwa na Chuo Kikuu cha Harvard ujulikanao kama Harvard Health Leaders' Ministerial Roundtable uliofanyika Geneva leo. 
Mkutano huo wenye lengo la kujenga uwezo wa Mawaziri wa Afya na Wataalam kwa njia ya kubadilishana uzoefu umehudhuriwa na mawaziri wa Afya kutoka nchi zaidi ya 40 wakiwemo Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo. 
Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Rais Mstaafu alialikwa kushiriki na kuelezea uzoefu wake katika mjadala kuhusu 'Mafanikio ya Kukumbukwa kwa Kuwezesha Utekelezaji wenye Matokeo' (Achieving a Legacy in Goverment by Getting Things Done). Katika mjadala huo, 
Rais Mstaafu Kikwete alielezea uzoefu wake kuhusu changamoto za utekelezaji wa programu na miradi ya Serikali na chimbuko la kuanzishwa kwa 'Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa' (BRN) ikiwemo mafanikio na changamoto zake. Katika jopo hilo, walishiriki pia Mhe. Baroness Tessa Jowel, Waziri wa Zamani wa Uingereza wa Masuala ya Olimpiki na Waziri wa Utamaduni, Michezo na Habari, na Mheshimiwa Idris Jala, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia anayeshughulikia Mpango wa Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Programu na Matokeo Malaysia ujulikanao kama PEMANDU.
Mheshimiwa Rais Mstaafu ameelezea changamoto aliyoipata kabla ya kuansishwa kwa BRN ambapo ilikuwa vigumu kujua na kufuatilia kwa uhakika hatua inayopigwa katika utekelezaji wa miradi na shughuli za Serikali. Kiu yake ilipata jawabu alipofanya ziara nchini Malaysia na kujifunza namna Mpango wao wa PEMANDU ulivyokuwa ukifanya kazi. 
Aliamua kujifunza kuwaalika wataalamu wa PEMANDU kuja kusaidia wataalam wa Tanzania kubuni mpango wa BRN. Ameusifia mpango wa BRN kuwa umewezesha ufanisi kwa kuwezesha kupata 'matokeo makubwa kwa rasilimali zile zile'. 
Aidha mpango umewaleta pamoja wadau wote wa ndani na nje ya Serikali kushirikiana pamoja na kuainisha changamoto, kukubaliana vipaumbele, ufumbuzi, kugawana majukumu na kuhimizana katika kutimiza wajibu wa kila mdau. Aidha imewezesha kuwepo kwa takwimu na uwazi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na uwajibikaji wa Serikali katika kutekeleza ahadi zake. Pamoja na uzuri wa mpango huo na mafanikio yaliyopatikana, changamoto kubwa ilikuwa ni upatikanaji wa rasilimali katika kutekeleza miradi hiyo kwa wakati. 
 Katika mjadala huo, Mawaziri wa nchi za Afrika wamevutiwa na uzoefu wa Tanzania na Mpango wa BRN na wameonyesha shauku ya kutaka kujifunza zaidi juu ya mpango wa BRN. Wamempongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa kuonyesha uongozi kwa kuwezesha ubunifu katika utekelezaji wa programu za Serikali ambao umekuwa na matokeo mazuri yenye kupimika.
Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akifafanua jambo  katika Mkutano wa Masuala ya Afya wa Mawaziri unaoandaliwa na Chuo Kikuu cha Harvard ujulikanao kama Harvard Health Leaders' Ministerial Roundtable uliofanyika Geneva leo. Wengine ni Mhe. Baroness Tessa Jowel, Waziri wa Zamani wa Uingereza wa Masuala ya Olimpiki na Waziri wa Utamaduni, Michezo na Habari, na Mheshimiwa Idris Jala, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia anayeshughulikia Mpango wa Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Programu na Matokeo Malaysia ujulikanao kama PEMANDU.
Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwenye mkutano huo. Kushoto ni  Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo. 
Balozi Modest Melo akiwa na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo mkutanoni
Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo.