Monday, May 09, 2016

ADC Yawafuta Wanachama wake Wanne Akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho



ADC Yawafuta Wanachama wake Wanne Akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho
Chama cha Alliance for Democratic Change ADC kimewafuta uanachama wanachama wake wanne akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Bwana Said Miraaj,Katibu Mkuu Bi.Lydia Bendera,Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi Bwana Jumanne Magafu pamoja na Katibu wa Kamati ya ulinzi Bwana Juma Wandwi kwa makosa ya kukiuka katiba ya chama hicho kwa kususia kushiriki uchaguzi mkuu wa marudio wa Zanzibar.

Maamuzi hayo yamefikiwa katika mkutano mkuu wa chama hicho ambapo akizungumza baada ya ufunguzi aliyekuwa mlezi wa chama cha ADC ambaye pia ni Waziri wa Kilimo Zanzibar,Mhe.Hamad Rashid amesema katiba ya chama inasisitiza ushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,hivyo kutoshiriki ni kukivunja nguvu chama katika mikakati yake ya kuchukua dola.

Akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa -ADC- Msajili Msaidizi wa vyama vya siasa Bwana Sisty Nyahoza amesema kitendo cha chama cha siasa kutoshiriki uchaguzi kinakwenda kinyume na sheria ya vyama vya siasa na malengo ya kuanzishwa chama Chochote cha siasa na kusisitiza ipo haja ya kuangalia mfumo wa usajili wa vyama utakaowezesha kutoa adhabu kwa vikavyoonekana kukataa kushiriki katika chaguzi.

Aidha katika mkutano mkuu huo, wajumbe wamemchagua aliyekuwa mlezi wa ADC ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo Zanzibar Mhe.Hamad Rashid kuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bwana Doyo Hassan Doyo amechaguliwa kushika wadhifa wa katibu mkuu wa chama.