Tuesday, April 19, 2016

WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI YAENDELEA NA UTATUZI WA MIGOGORO



WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI YAENDELEA NA UTATUZI WA MIGOGORO
Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula amesema, huduma bora ni haki ya wananchi na kufanya kazi kwa weledi ni wajibu wa watendaji wa Serikali. Naibu Waziri aliyasema hayo alipofanya mkutano na wananchi pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba katika ukumbi wa St. Francis.

Katika mkutano huo na wananchi, Naibu Waziri Mhe. Mabulla alipokea kero/malalamiko ya wananchi ambapo, baadhi yake yalipatiwa majibu hapo hapo na mengine kuamriwa yapatiwe majibu ndani ya wiki mbili. Maagizo hayo yalitolewa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kwa kushirikiana na Katibu Tawala Wilaya ya Bukoba.

Pamoja na kutoa tamko kwa Mkurugenzi na watendaji wa Manispaa ya Bukoba, pia aliwaasa watendaji kujipanga namna ya kufanya kazi kwa kuangalia jamii wanayoihudumia. Alitolea mfano wa wazee ambao hawana uwezo tena wa kuhangaika na kero za sekta ya ardhi katika maeneo yao.  Alisema, kila mtendaji akifanya kazi yake kwa kujituma na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, haki na usawa vitakuwepo na migogoro haitakuwepo tena.