WAZIRI wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema kuwa ,Serikali imendaa Muswada wa kutungwa kwa Sheria ya Wazee ambayo itapelekwa Bungeni ili ipitishwe kuwa sheria itakayosimamia upatikanaji wa haki na ustawi wa wazee wote nchini.
Waziri Mwalimu ,alisema leo Aprili 6, mwaka huu katika hotuba yake ya uzinduzi wa Kitaifa wa Kampeni ya ' Mzee Kwanza – Toa Kipaumbele apate huduma kwanza ilizunduliwa katika ukumbi wa bwalo la Umwema mjini Morogoro.
Amesema muswada wa kutungwa kwa sheria hiyo unatarajiwa kuwasilishwa mbungeni mnamo Septemba mwaka huu ambapo sheria hiyo itatoa ahueni kubwa kwa wazee na kuboresha maisha yao ya uzeeni.
Pamoja na kuandaliwa kwa muswada huo, Waziri Mwalimu kwa niaba ya Serikali imeagiza kila Halmashauri nchini kubaini wazee walio katika maeneo yao na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na huduma za afya kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri hizo.
Waziri Mwalimu alitumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wote wa Halmashauri mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa jambo hilo linasimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi wote. "Serikali ilipitisha maamuzi kwamba wazee watatibiwa bure katika maeneo yao ...najua utekelezaji wa hili haujawa mzuri kwa baadhi ya maeneo" alisema Waziri Mwalimu na kuongeza.
" Ni chukue fursa hii kuagiza kila taasisi ama asasi inayotoa huduma yoyote kutenga dawati maalumu la kuhudumia wazee wanaokuja kupata huduma " alisisitiza Waziri Mwalimu. Waziri alisema ,Kampeni ya Mzee kwanza ni kwa kila Mtanzania, hivyo viongozi wa ngazi mbalimbali wa taasisi na asasi wanatakiwa kuweka mikakati na ubunifu kuhakikisha wazee popote walipo wanapewa vipaumbele katika huduma za kijamii. Waziri alitoa hamasa kwa Taasisi , Mashirika na Asasi mbalimbali pamoja na wananchi kuunga mkono na kushiriki kikamilifu katika kampeni ya Mzee Kwanza . Alisema , Serikali ya awamu ya tano imeona na kutambua umuhimu wa wazee katika ujenzi wa taifa na kutambua mchango wao makubwa kwa nchi yao ambao umeifanya Tanzania ionekane vyema katika ramani ya dunia.
" Ili kutekeleza dhamira hiyo ya kuwajali wazee, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk John Magufuli ameunda Idara maalumu ya kuhudumia wazee na kuiweka chini ya Wizara yangu nami napenda kuwahakikishia wazee wa Tanzania nzima kuwa sitawaagusha" alisema Mwalimu . Pia Waziri Mwalimu alitumia fursa hiyo kumpongeza mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli kwa moyo wake wa kuwajali wazee wasiojiweza na kuwasaidia vifaa katika vituo mbalimbali nchini jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono na jamii ya watanzania ya kuwaenzi na kuwajali wazee . Naye Kaimu Mkurugerenzi mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) , Michael Mhando, alisema NHIF imeweka msukumo kuhusu masuala ya wazee ikiwemo kupitia Kampeni ya Mzee kwanza .
Alisema, kwa busara Bosi ya Mfuko na Uongozi uliokuwepo wakati ule, ukaone ni vema kuanzisha utaratibu wa kuwapa huduma za matibabu wanachama wastaaafu na weza wao kwa maisha yao yote baada ya kutoka kwenye utumishi wa umma. Mhando alisema kuwa, hadi kufikia Desemba mwaka jana ( 2015) , Mfuko ulisajili wanachama wastaafu 27,056 , lakini pia unawahudumia wanachama wastaafu 51,598.
Hivyo alisema kufuatia mpango huo, Mfuko utakuwa bega kwa bega na wizara katika kampeni hiyo ya Mzee Kwanza na kumwomba Waziri kuwaagiza watoa huduma hususani za afya nchini kutoa kipaumbele cha huduma kwa wazee. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF alisema , pamoja na hilo, Mfuko utaendelea kuhimiza watoa huduma za afya kutoa kipaumbele kwa wazee katika dirisha maalumu la huduma kwa wanachama wa Bima ya Afya.
Naye Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe, alisema Ofisi yake itafuatilia kwa karibu zaidi maendeleo ya kampeni hiyo na utoaji wa huduma bora za afya kwa wazee katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na nyingine za wilaya mkoani humo. Dk Kebwe alisema , hatua hiyo ni kuona mpango huo unawanuaisha wazee katika kupata huduma bure za afya kama lililokusudiwa na Serikali ya kutoa matibabu bure kwa wazee wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea.
Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,akizungumza na wazee wa Mkoa wa Morongoro juu ya uzinduzi wa Kitaifa wa Kampeni ya ' Mzee Kwanza – Toa Kipaumbele apate huduma kwanza ilizunduliwa katika ukumbi wa bwalo la Umwema leo Mkoani Morogoro.kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe
Mkurugerenzi mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) , Michael Mhando, akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Morogoro juu ya msukumo kuhusu masuala ya wazee ikiwemo kupitia Kampeni ya Mzee kwanza, leo Mkoani Morogoro
Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akipoke zawadi kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Mtandao wa Maendeleo ya Wazee Tanzania Wilson Karuwesa, leo Mkoani Morogoro
Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akipokea zawadi kutoka kwa wamama wa Mkoa wa Morogoro, leo
Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizinduwa Kampeni ya ' Mzee Kwanza – Toa Kipaumbele apate huduma kwanza ilizunduliwa katika ukumbi wa bwalo la Umwema leo Mkoani Morogoro.
(Picha na Emmanuel Massaka wa Globu ya Jamii)