Saturday, April 23, 2016

Wahandisi Temesa watunukiwa vyeti



Wahandisi Temesa watunukiwa vyeti
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme(TEMESA) Mhandisi Manase Ole Kujan, amewatunuku baadhi ya waandisi na mafundi  wakati  akifunga mafunzo ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology) kwa watumishi wa TEMESA.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa wiki mbili, yametolewa kwa kushirikia na chuo kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha Fizikia, kwa watumishi 20 wa TEMESA kupata mafunzo ya nadharia na vitendo.

Katika hotuba yake Mhandisi  Manase aliushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuendesha mafunzo hayo kwa wataalamu wa TEMESA, kwani yatawapa uwezo wahandisi na mafundi wa kuendana na mabadiliko ya sayansi na tekenolojia.

"Nishati ya umeme wa jua imeshika kasi kwa sasa na inatumiwa sana katika maeneo ambayo umeme wa kawaida haujafika hivyo basi kwa mafunzo haya wahandisi na mafundi wetu wataweza kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuandaa na kutekeleza miradi itakayosaidia kuondokana na tatizo la umeme nchini." Alisema Mhandisi Manase.

Aidha, TEMESA inasimamia miradi mbali mbali ya teknolojia ya umeme wa jua nchini ikiwemo mfumo wa teknolojia ya umeme wa jua kwa shirika la utangazaji Tanzania (TBC) Songea, mfumo wa teknolojia ya umeme wa jua katika ofisi ya Rais Utumishi, kusimamia na kuhakiki mifumo ya  teknolojia ya umeme wa jua inayofungwa  vijijini katika mikoa ya Geita, Kigoma Ruvuma na Tabora iliyo chini ya REA, kusimamia matengenezo ya mifumo ya teknolojia ya umeme wa jua katika ofisi zote za TRA pamoja na miradi mbali mbali ya taa za kuongozea magari barabarani zinazotumia teknolojia ya umeme wa jua.
Dr. Brenda Kazimili kutoka kitengo cha Fizikia Chuo kikuu cha Dar es Salaam, akielezea umuhimu wa mafunzo ya teknolojia ya Umeme wa Jua(Solar Photovoltaic Technology) yaliyotolewa kwa Watumishi wa TEMESA wa tatu kulia ni Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan.
Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan akikabidhi cheti kwa Mhandisi Amani Mwanga baada ya kuhitimu mafunzo ya teknolojia ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology)
Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Manase Ole Kujan akikabidhi cheti kwa Mhandisi Sara Moses baada ya kuhitimu Mafunzo ya teknolojia ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology).
Mtendaji Mkuu TEMESA Mhandisi Manase OleKujan ( wa sita kulia waliosimama) akiwa kwenye picha ya pamoja na wahitimu wa Mafunzo ya teknolojia ya umeme wa jua (Solar Photovoltaic Technology) kutoka TEMESA. (Picha Zote na Theresia Mwami wa TEMESA).