Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza katika siku ya tatu ya Mkutano Maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mafanikio na changamoto za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya duniani.
Sehemu ya Washiriki wa Mkutano Maaluma wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu dawa za kulevya.
Balozi Tuvako Manongi ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu akiwa na Bw. Rogers William Siyanga na Bw. Khamis Abdalla muda mfupi kabla ya kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokutana kujadili changamoto za dawa za kulevya. Mkutano huo umemalizika siku ya Alhamis.
Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema, waathirika wa dawa haramu za kulevya wanatakiwa kusaidiwa badala ya kuwafunga jela.
Hayo yameelezwa jana ( Alhamis) na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, katika Mkutano Maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliokuwa ukijadili mafanikio, juhudi na changamaoto za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya duniani.
Balozi Manongi ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu wa siku tatu na ambao umewashirikisha Viongozi Wakuu wa Nchi, Serikali na Mawaziri kutoka mataifa mbalimbali.
"Tunapoangalia mbele, mkazo wetu uwe katika kuhakikisha tunapunguza idadi ya watu wanaojihusisha na matumizi ya dawa haramu za kulevya na tunapunguza idadi ya watu wanaofariki kutokana na matumizi ya dawa hizo" akasema Balozi
Na kusisitiza " Lazima tuhakikishe wale wenye makosa madogo hawaishii jela ambako matatizo yao yatokanayo na dawa za kulevya yatazidi kuwa makubwa zaidi. Lakini pia tunao wajibu wa kuhakikisha huduma wanazopewa zinazingatia afya na haki za binadamu."
Mwakilishi huyo wa Tanzania, amewaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine Tanzania haijapona na balaa hilo la dawa za kulevya.
"Tanzania hatujasalimika na balaa hili, nchi yetu, imekuwa sehemu ya kupitisha dawa za kulevya kuelekea nchi nyingine. Lakini kiasi fulani cha dawa hizo kina baki nchini na hivyo kuathiri wananchi wetu ambao wengine wao tayari wameshaathirika kwa umaskini na matatizo mengine".akaeleza Balozi
Akasema, ni kweli kwamba, tatizo la dawa za kulevya, ni kubwa na lenye changamoto nyingi, na ni tatizo ambalo halina ufumbuzi wa mara moja, lakini pia ni tatizo ambalo lisiifanye jumuiya ya kimataifa kukata tamaa.
Akasema Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kupitia mkutano huo kuhakiksha kwamba inakuja na mikakati mipya ikiwa ni pamoja na kutekeleza yale yaliyopendekezwa kwenye tamko lililopitishwa kwenye mkutano huo. Balozi Manongi ameongeza kuwa hapana shaka sera na sheria zilizopo hivi sasa zimeshindwa kudhibiti wimbi la athari za dawa za kulevya. Na kwa kutambua ukubwa na changamoto za tatizo hilo na athari zake kwa wananchi wa Tanzania , Serikali imejiwekea mipango na mikakati mbalimbali ya kulikabili.
Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na kuwasaidia waathirika wa dawa za kulevya na ambao wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa na kuambukiza magonjwa mbalimbali yakiwamo ya virusi vya ukimwi na Hepatitis B na C,
Akaelezea pia juhudi zinazofanywa na serikali katika utungaji na uboreshaji wa sheria zinazolenga kuwabana wasafirishaji, wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo, ikiwamo mikakati ya kufuatilia kwa makini mwenendo mzima wa biashara ya dawa za kulevya , matumizi na matumizi ya madawa mengine ya aina hiyo.
Balozi Manongi amesema pia kwamba tatizo la dawa za kulevya linarudisha nyuma juhudi za pamoja na kuwapatia watanzania maisha yenye hadhi na inaathiri nguvu kazi ambayo inahitajika kufikia malengo ya kiuchumi na maendeleo ya jamii.
" Kama hiyo haitoshi dawa za kulevya zinachochea uhalifu na vitendo vya jinai vikiwamo vinavyohusisha ujagili wa wanyamapori na misitu, na kuongeza kazi ya ziada kwa vyombo vya sheria na mfumo wa kitaifa wa utoaji huduma za afya". Amesisitiza Balozi
Katika vita hivyo dhidi ya dawa za kulevya na umuhimu wa kuwasaidia waathirika, Balozi Manongi amesisitiza kwamba ushirikiano wa pamoja baina ya mataifa, taasisi za kimataifa na asasi zisizo za kiserikali unahitajika sana kwa kile alichosema hakuna nchi inayoweza kukabiliana na tatizo hilo peke yake.
Akaongeza pia kwamba utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa, utasaidia sana katika kuyakabili makundi na mitandao ya kihalifu na rushwa.
Hoja zilizopewa msisitizo na wazungumzaji wengi ni pamoja na hiyo ya kuwapatia waathirika matibabu na kutowafunga kwa kile walichosema hakuna mzazi anayependa kuona mtoto wake akifungwa na badala yake angefurahi kuona anasaidiwa.
Pamoja na kuzungumzia adhabu ya kuwafunga waathirika wa dawa za kulevya, wazungumzaji wengi pia wamepinga au kukemea adhabu ya kuwanyonga wanaokamatwa kuhusika na masuala ya mihadarati.
Aidha viongozi wengine walieleza kwamba wameanza mikakati ya kuwapatia wananchi wao hasa maskini utalaamu wa kulima mazao mbadala badala ya kutegemea kulima mazao yanayotumika kutengeneza dawa za kulevya kama sehemu ya kuendesha maisha yao.
Wengine wameeleza juhudi ambazo serikali zao zinafanya katika kukabiliana na mitandao na magenge wafanyabiashara wa dawa za kulevya , juhudi zinazohusisha pia kukamata na kutaifa mali zao.
Wako waliokwenda mbali Zaidi kwa kutaka nchi ambazo kwa namna moja ama nyingine zimelegeza sheria zao na kuruhusu matumizi ya dawa za kulevya kama vile bangi basi nazo ziwajibike kwa kutoa ushirikiano na kuonyesha utashi wa kisiasa.
Marais wanaotoka katika nchi ambazo zimeathirika zaidi na biashara za dawa za kulevya na mitandao ya kihalifu inayojihusisha na biashara hiyo, walikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa, ikiwa nchi zilizoendelea na ambazo ni wadau wakubwa hazitaonyesha ushirikiano ni wazi kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya itashindikana.