Friday, April 01, 2016

TANTRADE NA TAASISI YA TEKNOLOJIA YA DAR-ES-SALAAM, KAMPASI YA MWANZA WAANDAA MAFUNZO YA KUENDELEZA SEKTA NDOGO YA NGOZI



TANTRADE NA TAASISI YA TEKNOLOJIA YA DAR-ES-SALAAM, KAMPASI YA MWANZA WAANDAA MAFUNZO YA KUENDELEZA SEKTA NDOGO YA NGOZI
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ikishirikiana na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) - Kampasi ya Mwanza, inaandaa Mafunzo maalum ya wadau yanayolenga kuendeleza sekta ndogo ya Ngozi na bidhaa zake hapa nchini. Mafunzo haya yanatarajia kufanyika katika Taasisi hiyo kuanzia tarehe 18 - 22 Aprili, 2016 na yatahusisha Wajasiriamali wapatao 50, kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa.  
Katika muda wa siku tano (5), Washiriki watapata Mafunzo ya vitendo "Practical Training" ya namna ya kuandaa Ngozi katika mfumo mzima wa mnyororo wa thamani "value chain" hadi hatua ya kutengeneza kiatu "Basic Shoe Manufacturing  Course".  
Hayo yameelezwa na Bw. Edwin Rutageruka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TANTRADE wakati akiongea na Waandishi wa habari Jijini Mwanza hivi karibuni. 
Bw. Rutageruka alieleza kuwa Mafunzo haya yatatanguliwa na mafunzo maalum ya kuchuna ngozi za ngombe yatakayofanyika katika machinjio ya Vingunguti Dar-es Salaam kuanzia tarehe 11 – 15 Aprili 2016 na yatashirikisha wachuna ngozi 30.  
Lengo la mafunzo hayo ni kutekeleza vipaumbele vya TanTrade ikiwemo kuendeleza sekta ndogo ya ngozi  pamoja na vile vya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo ina mikakati ya kuongeza thamani ya bidhaa na  kuimarisha sekta ya viwanda hapa nchini.
Tanzania ina utajiri mkubwa wa mifugo barani Afrika. Tanzania ni nchi ya pili kwa utajiri wa mifugo ikiifuatia nchi ya Ethiopia. Takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa, Tanzania ina mifugo milioni 25. 8 ambapo, asilimia 97 ya mifugo yote hiyo ni mifugo ya asili. 
Pamoja na wingi huo, sekta ya mifugo ilichangia asilimia 4.4 ya pato la taifa mwaka 2013 ikiwa na kasi ya ukuaji waasilimia 3.8 tu. 
Aidha, asilimia 37 ya Watanzania wanategemea sekta hii kama shughuli yao kuu ya kiuchumi.  Zao la ngozi ni zao la mifugo muhimu ambalo likiendelezwa lina mchango mkubwa kwa wafugaji na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

  Bw. Edwin Rutageruka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TanTrade (kulia) akipata maelezo ya ushonaji wa kiatu toka kwa Fundi Anderson Magosha wakati alipotemblea karakana ya kutengeneza bidhaa za ngozi ya DIT Mwanza. Kushoto ni Dr Albert Mmari Mkuu wa Chuo hicho.
  Bw. Edwin Rutageruka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TanTrade akipata maelezo ya ushonaji wa viatu wakati alipotemblea karakana ya kutengeneza bidhaa za ngozi ya DIT Mwanza.