Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa ametoa pongezi kwa kampuni mpya ya simu ya Halotel kwa juhudi zake inazofanya katika kutekeleza mkakati wa kuhakikisha huduma ya mawasiliano inapatikana maeneo ya vijijini.
Pamoja na ongezeko la zaidi ya asilimia 16 la idadi ya watumiaji wa simu za mikononi nchini bado tatizo la upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa maeneo ya vijijini imekuwa ni changamoto.
Prof Mbarawa alisema serikali imekuwa inafanya juhudi mbalimbali ili kuziba pengo la upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kati ya maeneo ya vijijini na mijini, na hivyo mwaka 2006 mfuko wa mawasiliano kwa wote ulianzishwa kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na mijini.
'Kulikuwa na mwamko mdogo kutoka kwa makampuni ya simu katika kupeleka mawasiliano vijijini kutokana na mazingira yake na changamoto kama vile kuwa na idadi ndogo ya wakazi, ndio maana serikali ikaanzisha mfuko wa upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa wote ili kusaidia katika zoezi la utekelezaji wa upanuzi wa huduma ya mawasiliano' alisema Mbarawa.
Hata hivyo, Prof Mbarawa amebainisha kuwa bado mwitikio wa uombaji wa zabuni kwa ajili ya jitihada za kupanua mawasiliano maeneo ya vijijini umekuwa ni mdogo sana na hivyo basi kusababisha maelfu ya vijiji kukosa huduma ya mawasiliano na hivyo kuendelea kukithiri kwa hali ya umaskini .
'Wakati kampuni ya simu ya Halotel ilipokuja nchini na mkakati wa kuwekeza maeneo ya vijijini, sisi kama serikali tuliwapokea kwa mikono miwili na tukaahidi kuwasadia baadhi ya mambo ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo, lakini pia tukawapa masharti ya kuhakikisha wanaunganisha mawasiliano ya mtandao kwa ofisi za vijiji 150, hospitali za umma 150, vituo vya polisi 150, pamoja na ofisi za posta 65 na pia shule 450 'alisema Prof Mbarawa.
Hadi sasa, Kampuni ya simu ya Halotel kwa sasa imeunganisha huduma ya mawasiliano kwa vijiji 1800 ambavyo vilikuwa havina huduma hiyo, na kufikia mwishoni mwa mwaka huu kampuni ya simu ya Halotel itakuwa imeunganisha vijiji vingine 1500 kwa mara ya kwanza ili kuhakikisha huduma bora ya mtandao wa 3G.
'Kampuni ya Halotel imeunganisha zaidi ya watumiaji wa huduma ya simu 1,800, ambao kabla walikuwa hawajaunganishwa,na muhimu zaidi, wameunganishwa na mtandao wa kasi wa 3G kupitia fiba yenye kilomita 18,000 na hivyo kusaidia watumiaji wa huduma hiyo kupatikana mahali popote na kwa wakati wowote ' alisema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu ya Halotel, Le Van Dai.
Serikali ya Tanzania na mshirika wake Kampuni ya Halotel wamewekeza jumla ya dola za kimarekani billioni moja sawa na trilioni 2 za kitanzania katika kutekelezeka upanuzi wa huduma ya mawasiliano kwa mikoa mikoa 26, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa kuunganisha vijiji 1,500 kupitia mkonga wa mawasiliano unaovuka kilometa 2,500 pamoja na na kusambaza kilometa 18,000 za fiba nchini kote, na hivyo kuifanya kampuni ya simu ya Halotel kuwa mtandao ulionea zaidi nchini .