Tuesday, April 12, 2016

KAIMU MKURUGENZI MTENDAJI STAMICO AIPONGEZA STAMIGOLD KWA KUWA MGODI WA MFANO NCHINI



KAIMU MKURUGENZI MTENDAJI STAMICO AIPONGEZA STAMIGOLD KWA KUWA MGODI WA MFANO NCHINI
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa STAMICO Bi. Zena Kongoi ameupongeza mgodi wa STAMIGOLD Biharamulo uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera kwa kuendelea kuwa mfano wa mgodi pekee hapa nchini unaomilikiwa na serikali kwa 100% na kuzalisha dhahabu chini ya Wataalam wa Kitanzania pekee.

Pongezi hizo zilitolewa wakati wa ziara yake hapa mgodini mwishoni mwa juma iliyolenga kuzungumza na Wafanyakazi na kuelezea dhamira kuu ya STAMICO ya kuhakikisha mgodi huu unasonga mbele pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazoukabili mgodi hususani suala la ufinyu wa mtaji na kuahidi kuwa Shirika limepanga kwa mwaka huu wa 2016 fursa zote zinazohusu madini zinaunufaisha mgodi wa STAMIGOLD.
" Ningependa kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya pamoja na uwepo wa changamoto nyingi na hasa ya ufinyu wa mtaji lakini bado mnaendelea kutumia ubunifu na uzalendo wenu kuendesha mgodi na kuzalisha dhahabu hivyo kwa niaba ya STAMICO tunawapongeza sana na tunatambua kazi yenu nzuri mnayofanya ukizingatia kuwa moja ya malengo ya serikali ya sasa ni kuhakikisha uchumi wa madini unarudi kwa Watanzania na kwa kupitia mgodi huu mmeweza kuonyesha kuwa hilo linawezekana" Alisema Bi. Kongoi.

Bi. Kongoi aliongeza kuwa lengo kubwa la kuanzisha kampuni ya STAMIGOLD ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa ni kuhakikisha inasimamia maslahi yote ya dhahabu kwa niaba ya Shirika hivyo mgodi wa Biharamulo ukifanikisha lengo hilo ni mwanzo wa kufufua migodi mingine ya dhahabu nchini mfano Buhemba na Buckreef ambapo tayari STAMIGOLD imekuwa ikitoa msaada hasa wa kitaalam katika mipango ya kufufua mgodi wa Buhema uliopo mkoani Mara.
Vilevile alisisitiza Wafanyakazi kushirikiana vizuri na Menejimenti ya mgodi katika kufikia malengo yaliyowekwa na mgodi na kuweka njia mbalimbali za kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi pamoja na Kitengo cha Mawasiliano kuongeza kasi katika kuutangaza mgodi.

Wafanyakazi walipata wasaa wa kuuliza maswali pamoja na kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali hususani suala la mgodi kuwezeshwa kiuchumi ili kuweza kufikia malengo ya uzalishaji na kuongeza uhai wa mgodi ambapo yote yalipokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na kutolewa ufafanuzi akishirikiana na Kaimu Mkurugenzi Rasilimaliwatu na Utawala STAMICO Ndg. Deusdedit Magalla ambaye aliahidi kushirikiana na Kitengo cha Rasilimali Watu hapa mgodini kuhakikisha pale zinapotokea fursa za ufadhili wa mafunzo mbalimbali ya kitaalam zinazotolewa chini ya Wizara ya Nishati na Madini pamoja na taasisi mbalimbali zinanufaisha pia wafanyakazi wa mgodi.
Watendaji hao wa STAMICO kwa pamoja walipata wasaa wa kutembelea kliniki ya mgodi na kuelekea katika maeneo ya uchimbaji ya West zone na Mojamoja ambapo shughuli za uchimbaji dhahabu zinapofanyika na baadae kutembelea mtambo wa kuchenjulia dhahabu (Process Plant).

Hii ni mara ya kwanza kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bi. Zena Kongoi kuzungumza na wafanyakazi wa STAMIGOLD tangu alipopata wadhifa huo mara baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa Mhandisi Edwin Ngonyani kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwishoni mwa mwaka 2015.