Monday, March 21, 2016

Waziri wa Uingereza atembelea kambi za wakimbizi Tanzania


Waziri wa Uingereza chini ya Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID)-Anayeratibu Masuala ya Afrika, Ndugu Nick Hurd MP, amewasili Tanzania asubuhi hii kwa ziara fupi mjini Kigoma.

Waziri atatembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, moja ya kambi kubwa sana ya wakimbizi duniani. Nyarugusu ina wakimbizi zaidi ya 140,000 warundi na wakongo ambao wamekimbia mapigano toka nchini mwao kwa zaidi ya miongo miwili. Waziri pia atakutana na viongozi wa serikali za mitaa na mashirika ya misaada ya kibinadamu ambao wanafanya kazi katika maeneo hayo.

Waziri alisema: "Tanzania ni wakarimu sana kwa kuwakubalia zaidi ya wakimbizi 130,000 warundi ambao wamekimbia vurugu na mauaji nchini mwao. Uingereza nayo itatoa mchango wao pia. Sisi ni miongoni mwa wahisani wakubwa walioitikia na kuendelea kusaidia Tanzania na UNHCR wanavyoendelea na shughuli zao.

Hivyo, ni muhimu sana kwangu kuwepo hapa kujionea maendeleo na changamoto ambazo zipo. Lakini pia hizi ni nyakati ambazo kuna changamoto kubwa ya wakimbizi duniani, nataka kutoa rai kwa jumuiya za kimataifa kuongeza misaada yao katika janga hili lisilozungumzwa sana"

Tangu Aprili, 2015 zaidi warundi 252,000 wamekimbia machafuko ya kisiasa nchini mwao. Zaidi ya nusu - 133,000 – wameingia Tanzania. Kwa wastani, zaidi ya wakimbizi 1000 huingia kila wiki. Wakimbizi wanapata hifadhi katika kambi tatu; kubwa kuliko zote ikiwa ni kambi ya Nyarugusu ambayo inatembelewa na Waziri katika zaira yake.

Nyarugusu inahudumia wakimbizi takribani 65,000 wakongo na vilevile wakimbizi warundi 80,000. Kambi nyingine zikiwa ni Nduta (yenye wakimbizi 50,000) na Mtendeli (yenye wakimbizi 5,000) Uingereza ni moja ya wahisani wakubwa katika baa la wakimbizi wa Burundi.

DFID imetoa Paundi 14.25 milioni kwa Tanzania na kufanya kazi na serikali ya Tanzania na mashirika ya misaada ya kibinadamu. Ruzuku za Uingereza zimewezesha kupatikana kwa maji safi ya kunywa, vyoo, makazi, chakula, na huduma za afya kwa wakimbizi wakirundi elfu ambao wanaishi katika makambi Magharibi mwa Tanzania.