Picha ni mnyama aina ya                kasa ambaye anapatikana katika hifadhi ya taifa ya saadani                iliopo mkoani Pwani 
        Na Woinde Shizza Pwani.
        VIUMBE wa baharini aina                ya kasa wametajwa kuwa miongoni mwa viumbe wanaoishi                katika mazingira hatarishi huku wakitajwa kuwa wako                hatarini kupotea duniani kutokana na shughuli za binadamu                na mabadiliko ya tabia nchi.
        Hayo yamesemwa na                mtaalamu wa kasa katika hifadhi ya taifa ya Saadan iliyopo                Bagamoyo mkoani Pwani,Hamis Abdallah wakati akizungumza na                waandishi wa habari waliotembelea katika hifadhi hiyo                kujifunza vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani ya                hifadhi hiyo.
        Akiongea na waandishi                  wa habari jana mtaalamu huyo alisema ya kwamba baadhi ya                  wavuvi wamekuwa wakihatarisha maisha ya viumbe hao                  wanaopatikana kandokando ya bahari ya Hindi inayopakana                  na hifadhi hiyo kutokana na kuwavua hovyo .
                          Alisema kwamba kasa                      huzaliana nchi kavu na ndiyo maana amekuwa                      akijijengea baadhi ya maadui ambapo aliwataja kuwa                      ni papa,kenge ambao wamekuwa wakishambulia mayai yao                      na kutishia uhai wa viumbe hao.
                "Kasa wanaishi                      katika mazingira magumu sana kwa kuwa wanaishi                      katika kina kifupi cha maji na hivyo baadhi ya                      wavuvi huwavua hovyo lakini pia wana tabia ya                      kuzaliana nchi kavu na sio majini"alisema mtaalamu                      huyo.
                Hatahivyo,alisisistiza                      ya kwamba kutokana na tishio la kutoweka kwa viumbe                      hao hifadhi ya taifa ya Saadan imechukua hatua za                      haraka kuhakikisha wanachukua eneo kubwa la bahari                      ili kuwahifadhi viumbe hao sanjari na kutunza                      mazingira katika eneo hilo.
                Alisema kuwa                      hifadhi yao kupitia kitengo cha ujirani mwema                      kimekuwa kikishirikiana na jamii inayoizunguka                      hifadhi hiyo kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha                      kuhusu kutunza mazingira kwa lengo la kutoathiri                      mabadiliko ya tabia nchi kwa maslahi ya viumbe hao.
                "Tushirikiane                      kutunza mazingira ili kuhifadhi hawa viumbe wa                      baharini kwa kuwa wana faida kubwa sana kwa taifa                      endapo tutaendelea kuwatunza kasa hawa"alisisitiza                      Abdallah
                Hatahivyo,mtaalamu                      huyo alifafanua kuhusu sheria za utunzaji wa viumbe                      wanaoishi baharini na kusema kwamba sheria nambari 9                      kifungu cha 12 inayohusu utunzaji wa mazingira ya                      baharini ina sema iwapo mwananchi atahusika na                      uharibifu wa viumbe walio hatarini kutoweka                      atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu hadi mine.
               
