Ubalozi wa Tanzania nchini Canada ulikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mabalozi wa nchi wanachama wa SADC ambao wana ofisi za Ubalozi mjini Ottawa, Canada. Mkutano huo ambao umehudhuriwa na mabalozi wote wanane wanaowakilisha nchi zao Canada ulifanyika katika makaazi rasmi ya Balozi wa Tanzania hapa Ottawa, nchini Canada tarehe tarehe 15 Machi, 2016.
Nchi zilizowakilishwa ni Zimbabwe, Madagascar, Angola, Congo -DRC, Lesotho, Afrika ya Kusini, Zambia na Tanzania. Mbali na maswala mengine muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo mfupi wa siku moja agenda kubwa ya mkutano ilikuwa ni kuimarisha mshikamano wa kufanya kazi kwa pamoja ili kuziletea maendeleo nchi wanachama.
Aidha wanachama wa mkutanano hupata fursa ya kubadilishana taarifa za mambo mbalimbali yanayoendelea katika nchi zao. Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Canada Mhe. Jack Mugendi Zoka aliwaeleza Mabalozi wenzake juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano za kuinua hali za maisha ya watanzania hasa wenye hali ya chini kupitia kauli mbiu ya " Hapa Kazi Tu".
Balozi wa Zimbabwe nchini Canada ambaye ni Mwenyekiti wa Mabalozi wa SADC, Ottawa, Mhe. Florence Zano Chideya, akiweka saini katika kitabu cha wageni, mara baada ya kuwasili katika makaazi rasmi ya Balozi wa Tanzania, Ottawa, Canada.
Mabalozi wawakilishi wa SADC Ottawa, Canada wakiwa katika chumba cha mkutano, Tanzania House.
Balozi wa Tanzania nchini Canada, Mhe. Jack Mugendi zoka (kulia) akiwakaribisha rasmi mabalozi wenzake wa nchi za SADC, Tanzania House wakati wa ufunguzi wa mkutano huo. Kushoto ni Balozi wa Zimbabwe nchini Canada ambaye ni Mwenyekiti wa Mabalozi wa SADC, Ottawa, Mhe. Florence Zano Chideya.
Sekretarieti ya Mkutano wa SADC uliofanyika Tanzania House. Wa kwanza kutoka kulia ni Bw. Admire Hwata Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Zimbabwe, Wa katikati ni Bw. Leonce E. M. Bilauri, Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania, akifuatiwa na Bw. Liteboho K. Mahlakeng, Mkuu wa Utawala, Ubalozi wa Lesotho.
Pichani ya pamoja, Mbele wa kwanza kutoka kulia ni Mhe. Simon Constant Horace, Balozi wa Madagascar, Kulia kwake ni Mhe. Dr Mathabo Theresia Tsepa, Balozi wa Lesotho akifuatiwa na Mhe. Florence Zano Chideya, Balozi wa Zimbabwe nchini Canada ambaye ni mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za SADC. Aliyesimama kushoto mstari wa mbele ni Bw. Evaristo Kasunga, Kaimu Balozi wa Zambia. Balozi wa Tanzania Mhe. Jack Mugendi Zoka ambaye amesimama nyuma akiwa amevalia Tai ya bendera ya Taifa amepakana kulia kwake na Balozi wa Afrika ya Kusini Mhe.Membathisi Shepherd Mdladlana ambaye mbele yake ni Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bw. Kalelwa Kalimasi. Aliyesimama nyumba kabisa ya picha ni Mhe. Edgar Augusto Martins, Balozi wa Angola.