NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
SHIRIKA la ugavi wa umeme Tanesco Mkoani Pwani limewakamata watu saba kwa tuhuma za wizi wa umeme katika eneo la kwamfipa Wilayani Kibaha ambao walikuwa wamehujumu miundombinu kwa kujiunganishia umeme kinyemela kinyume cha utaratibu.
Akizungumzia kuhusina na tukio hilo Afisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Pwani Herny Byarugaba amesema kwamba kubainika kwa watu hao waliokuwa wanaiba umeme kumetokana baada ya kupatiwa taarifa kutoka kwa wananchi wasamalia wema wa eneo hilo.
Byarugaba amesema kwamba wezi hao walikuwa wamezichimbia nyaya za umeme chini ya barabara ya kuusambaza katika baadhi ya maeneo ikiwemo maduka, mabanda ya kuonenyeshea video hali ambao amedai ni hatari kwa usalama wa maisha ya watu kwani kunaweza kutokea majanga ya kuungua kwa nyuma za watu na kupoteza maisha yao.
"Sisi tumepata taarifa hizi kutoka kwa wananchi wasamalia wema kwa hiyo sisi kama tanesco tukaamua kufanya msako mkali katika eneo hili la kwa mfipa na kuweza kukuta wateja wetu wameamua kutumia njia za kinyemela kwa kuiba umeme na mbaya zaidi nyaya wamezipitishia chini kabisa ya barabara hivyo hali hii ni hatari sana watu wanaweza kupoteza maisha,"alisem Byarugaba.
Aidha alibainisha kwamba kutokana na kujiunganishia umeme kinyume na taratibu kunaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi kwani pindi mvua inaponyesha na nyaya hizo zikiwa zimechunika maji yanashika umeme na hivyo kunaweza kusababisha hatari kubwa sana.
Pia Byarugaba aliongeza kuwa Shirika la Tanesco limekuwa linapata hasara kubwa na kupoteza mapato yake kutokana na baadhi ya watu kuamua kufanya vitendo vya hatari vya kuhujumu miundombinu yao pamoja na kuiba umeme.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya mtaa kwamfipa Juma Tanga ambaye alifika eneo la tukio alisema kwamba amesikitishwa sana kuona baadhi ya wananchi wake kushiriki kuiba umeme kinyume na taratibu na kuwataka waachane na vitendo hivyo kwani ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba katika kukabiliana na hali hiyo atahakikisha anaweka mikakati ya kuwaelimisha wananchi wake katika mikutano mbali mbali kuhusina na madhara ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na kujiunganishai umeme bila ya kuzingatia taratibu zilizowekwa na wahusika wenyewe.
Naye Meneje wa Tanesco Mkoa wa Pwani Martin Madulu ametoa tahadhari kwa wananchi wote wa Mkoa wa Pwani kuachana kabisa na tabia ya kujiunganishia umeme pasipo kuwatumia wafanyakazi husika wa tanesco na badala wake wahakikishe wazingatie taratibu katika kuunganishiwa umeme katika sehemu za biashara pamoja na nyuma za kuishi.
Aidha katika hatua nyingine Mejeja huyo aliwataka wananchi kujihadhari ya matapeli ambao wanajifanya ni wafanyakazi wa shirika hilo na endapo wakiwabaini watoe taarifa mapema katika vyombo vinavyohusika ili sheria iweze kufuata mkondo wake.
Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika hilo wakiwa katika eneo hilo mara baada ya kubaini kuwepo kwa wizi huo wa umeme(PICHA NA VICTOR MASANGU).
Afisa Usalama wa shirika la ugavi wa umeme Tanesco Mkoa wa Pwani Henry Byarugaba akionyesha moja ya eneo ambalo wameiba umeme kwa kujiunganishia bila ya kuzingatia taratibu.