Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imefafanua kwamba uchunguzi wao umeonyesha kwamba Mke wa Rais, Mama Janet Magufuli hana akaunti ya Facebook na tovuti inayohamasisha watu kuomba mikopo ya vikundi vya Vicoba.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dr Ally Simba amesema Dar Es Salaam Jumamosi Machi 19 kwamba akaunti ya face book ambayo iliyodaiwa kuwa ni ya Mama Janet ilianzishwa na matapeli wa mtandao.
Dr. Simba alisema TCRA imeshafungia akaunti hiyo ya Facebook na tovuti ya www.focusvikoba.wapka.mobi ambayo ilikuwa ina tarifa za kutaka wananchi kutuma pesa za kiingilio kwa Vicoba ili wapate mikopo.
Dr. Simba alisema ingawaje kumekuwepo na maendeleo na mabadiliko makubwa katika sekta ya mawasiliano nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watoa huduma za mawasiliano, idadi ya watumiaji na aina ya huduma zinazotolewa kuna watumiaji wachache wanaotumia huduma hivyo kutenda uhalifu kupitia simu za mkononi na kwenye intaneti kwa kuanzisha tovuti za kihalifu na kupitia mitandao ya kijamii kama vile face book.
Alisema hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wahalifu hawa wa mtandao kuanzisha tovuti na blogu na pia kurasa za facebook kwa kutumia majina ya viongozi wakuu wa nchi, wabunge na watu wengine maarufu.
Wahalifu hawa wanawadanganya wananchi kwamba kuna fursa za kupata mikopo au misaada kupitia vikundi vya kusaidiana, maarufu kama VICCOBA na kuwataka wananchi watume fedha za kujiunga na huduma hizo kwa njia za simu za mkononi.
Alisema pamoja na kuzifungia akaunti hizo za facebook na tovuti, Mamlaka inashirikiana na Polisi kuchunguza matukio hayo na tayari hatua kubwa imefikiwa katika kuwakamata na kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya sheria. Mkurugenzi Mkuu alisema kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 15 (1) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015, mtu yeyote haruhusiwi, kwa kutumia kompyuta, kujifanya yeye ni mtu mwingine15.
Adhabu kwa kutenda kosa hili imeainishwa kwenye kifungu cha 15 (2) ambacho kinasema mtu akipatikana na hatia anaweza kutozwa faini ya isiyopungua shilingi milioni TANO au mara tatu ya thamani ya kile ambacho amekipata kupitia ulaghai huo, au kiasi ambacho ni kikubwa kati ya faini na mara tatu ya alichokipata. Vilevile anaweza kufungwa kifungo kisichopungua miaka SABA au vyote.
Uchapishaji wa taarifa za uwongo ni kosa chini ya Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015. Kwa mujibu wa kifungu hicho, mtu yeyote ambaye anachapisha taarifa kwa kutumia mfumo wa kompyuta akijua kwamba taarifa alizochapisha sio za kweli, ni za udanganyifu na sio sahihi na kwa lengo ka kukashifu, kutishia, kutukana,kudanganya na kuptosha umma anatenda kosa ambalo adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni TANO au kifungo miaka mitatu au vyote.
Dr. Simba aliwaomba wananchi kwa ujumla na hasa watumiaji wa huduma za mawasiliano kuzingatia sheria wanapotumia huduma za mawasiliano.
Aidha aliwataka Watanzania kuwa macho dhidi ya utapeli kupitia mitandao ya kijamii, tovuti na blogu ambazo zinawataka kutuma fedha au kuchangia kitu chochote ili wapewe mikopo au misaada. Wananchi wakiona matangazo ambayo wanayatia shaka, wawasiliane na Mamlaka ya Mawasiliano kwa taarifa zaidi.
Kuhusu maendeleo ya sekta, alisema hadi Desemba 2015, idadi ya laini za simu za mkononi ilikuwa 39,808,419 ukilinganisha na 2,963,737 mwaka 2005. Watumiaji wa intaneti walifikia 17,263,523 Desemba 2015 ukilinganisha na 1,013,104 mwaka 2005.