MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mahmoud Hashim Kambona amewataka wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) ili wapate matibabu pindi wakiugua .
Akizungumza kwenye uzinduzi wa uhamasishaji wa kujiunga na CHF uliofanyika mji mdogo wa Mirerani, Kambona alisema kaya nyingi zinatakiwa kujiunga na mfuko huo kwani unalipa sh10,000 na kutibiwa kwa mwaka mmoja.
Alisema wilaya ya Simanjiro ina utajiri wa kutosha ikiwemo madini, mifugo na ardhi nzuri yenye rutuba inayofaa kwa kilimo na kupitia rasilimali hizo jamii hiyo inapaswa kujiunga na mfuko huo ambao utawasaidia kujitibu pindi wakiugua.
"Pamoja na hayo japokuwa wilaya yetu ni tajiri kuliko wilaya nyingine kwa hapa nchini, lakini wananchi wetu maisha yao wanayoishi ni ya hali ya chini,hivyo msaada pekee wa matibabu ni kujiunga kwa wingi na CHF," alisema Kambona.
Alisema kaya nyingi zikijiunga na mpango huo zitasababisha hata dawa kupatikana kwa wingi kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo maeneo mbalimbali kutoka bohari kuu ya dawa (MSD) hivyo wajiunge kwa wingi.
Mkurugenzi wa uendeshaji wa (NHIF) Raphael Mwamoto alisema CHF ni utaratibu unaoilenga jamii kwenye maeneo ya halmashauri na wanachotakiwa ni kuchangia kati ya sh5,000 au sh10,000 au sh15,000 kiwango kinachopangwa na wilaya husika.
"Mfano hapa Simanjiro kaya huchangia sh10,00 na baada ya kutoa fedha hizo, serikali nayo inaongeza malipo yanayoitwa tele kwa tele kwa kiasi hicho cha sh10,00 kwa kila kaya, kwa ajili ya kupata tiba," alisema Mwamoto.
Alisema kinachotakiwa hivi sasa ni halmashauri husika kuweka miundombinu vizuri na kuboresha huduma za afya ikiwemo dawa na vifaa tiba, ili jamii ihamasike kuchangia mfuko huo kwa kuona inanufaika na mfuko huo.
Mkurugenzi uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Raphael Mwamoto akizungumza kwenye uhamasishaji wa wananchi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwa kaya ya watu sita kuchangia shilingi 10,000 na kupata matibabu kwa mwaka mmoja.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mahmoud Hashim Kambona akizungumza na wananchi wa Mji mdogo wa Mirerani, juu ya kujiunga kwa wingi na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwa kila kaya kulipa shilingi 10,000.
Baadhi ya wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakijiung ana mfuko wa afya ya Jamii (CHF) ambapo kaya yenye watu sita yaani baba, mama na watoto wane wanajiunga kwa shilingi 10,000 na kupata matibabu kwa mwaka mmoja.