Na Mwandishi Maalum, New York
Wajumbe wa Mkutano wa 60 wa Kamisheni kuhusu hali ya wanawake, wanaendelea na majadilino juu ya dhima ya uwezeshwaji wa wanawake na uhusiano wake katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030).
Akichangia majadiliano hayo,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ( Mb) anasema Tanzania inatambua kwamba uwezeshwaji wa mwanamke na mtoto wa kike ni muhimu sana katika kufanikisha utekelezaji wa Agenda 2030.
Na kwamba ili kufanikisha hilo, Serikali inaendelea na jukumu la kuhusisha na kuingiza Ajenda 2030 katika mifumo iliyopo ya kisera, mipango na mikakati ya kitaifa ya maendeleo.
Waziri Ummy Mwalimu anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu, amebainisha pia kwamba Serikali inapitia kwa makini lengo namba tano la agenda 2030 ambalo linazungumzia umuhimu wa kufanikisha usawa wa kijinsi na uwezeshaji wa wanawake wote na wasichana.
Akaeleza zaidi kwamba uamuzi wa serikali kufanya marejeo ya mikakati Na mipango ya kitaifa inalenga kuhakikisha kwamba usawa wa jinsia na uwezeshwaji wa wanawake unaendelea kuwa kipaumbele cha nchi.
Vilevile amesema, ushiriki jumuishi umefanyika katika kubuni viashiria ambavyo vinaendana na mahitaji ya nchi na vinaweza kutumika mpaka ngani za chini katika upimaji wa utekelezaji wa Agenda 2030.
Katika kuelezea zaidi uzoefu wa Tanzania katika uwezeshwaji wa mwanamke na msichana wa kitanzania.
Waziri pia alianisha sheria mbalimbali zinazolimda mwanamke na mtoto wa kike dhidi ya ukatili au ubaguzi wa aina yoyote ile , kuanzishwa kwa mifuko na Banki za kuwawezesha wanawake kujipatia mikopo kwa riba nafuu, uboreshwaji wa huduma za afya hususani afya ya mama na mtoto pamoja na fursa sawa za ajira zenye staha na fursa za kujiajiri.
Pamoja na kueleza namna Serikali inavyoendelea kujipanga katika utekelezaji wa Agenda 2030, Waziri Mwalimu amesema ili utekelezaji huo uwe na mafanikio tarajiwa, ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja sekta binafsi utahitajika sana.
Na akatumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau hao ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika maeneo mbalimbali
Baadhi ya changamoto ambazo amesema Tanzania inakumbana nazo katika jukumu hilo la uwezeshwaji wa wanawake na wasichana pamoja na vikwazo vya kimila na kitamadani anavyokumbana navyo mwanamke na mtazamo hasi dhidi ya wanawake.
Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb.)wakati akitoa taarifa ya nchi katika Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake Duniani (CSW).
Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb.) akiwa Ubalozini New York na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Peter Serukamba (kushoto na Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mhe. Tuvako Manongi baada ya kuwasilisha taarifa ya nchi katika Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake Duniani (CSW).