Monday, March 21, 2016

Mfanyakazi wa DW aachiwa huru baada ya kutekwa nyara


Mfanyakazi wa DW aachiwa huru baada ya kutekwa nyara
Mfanyakazi wa kujitegemea wa  Deutsche Welle nchini Tanzania, Salma Said, alizuiliwa kwa muda wa siku mbili na watu waliomteka nyara katika eneo moja lisilojulikana. Kwa mujibu wa polisi, hatimaye aliachiwa huru jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili ya Machi 20. 

Mwandishi huyo alitekwa nyara Ijumaa ya Machi 18 katika Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam akitokea Zanzibar, ambako alikuwa aripoti  juu ya  uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumapili ya Machi 20,  lakini kutokana na taarifa alizozipata kwamba usalama wake uko hatarini na baada ya kuzungumza na Idara ya Matangazo ya Afrika ya Deutsche Welle mjini Bonn, alishauriwa aondoke visiwani Zanzibar na akaelekea jijini Dar es Salaam. Kulingana na familia yake, Salma hakufika jijini humo. 

Kwa mujibu wa polisi jijini Dar es Salaam, sababu za kutekwa nyara kwake, mahala alipokuwa akizuiliwa au ni kina nani waliofanya  kitendo hicho, ni mambo ambayo bado yanachunguzwa. Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro aliiambia DW kwamba: "Tumo katika kuchunguza na tutatoa taarifa kuhusiana na tukio hilo na nani walihusika hapo baadaye." 
Mkurugenzi Mkuu wa  Deutsche Welle, Peter Limbourg, alisema baada ya kupokea taarifa ya kuachiwa huru Salma Said kwamba: "Fikra zetu ziko pamoja  naye na tuna furaha kwamba mwenzetu yuko huru. Heshima ya wafanyakazi wetu  ni muhimu zaidi, hasa katika nchi ambako uhuru wa vyombo vya habari na wa kutoa maoni unaekewa vipingamizi. Tunataraji kwamba uchunguzi juu ya kisa hiki utakamilika na kuwekwa wazi." 

Salma Said ni mwandishi na ripota maarufu. Mwandishi huyu wa habari mwenye umri wa miaka 45 amekuwa akifanya kazi kama mwandishi wa kujitegemea  wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle tokea mwaka 2000. Pia huyaandikia magazeti kadhaa ya ndani nchini Tanzania na mitandao kadhaa ya kijamii. Aliwahi kushambuliwa mnamo miaka ya nyuma. Mwaka 2012, alishambuliwa na kikundi cha watu alipokuwa akitoka kuripoti juu ya mkutano  wa hadhara wa  chama cha upinzani mjini Unguja. 

Imetolewa na: 
Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle
Bonn
Ujerumani