Wednesday, March 23, 2016

Lolensia Bukwimba:Tamasha la Pasaka ni furaha iliyoje



Lolensia Bukwimba:Tamasha la Pasaka ni furaha iliyoje
MBUNGE wa Busanda (CCM) LOLENSIA BUKWIMBA ameeleza furaha yake kwa kamati maandalizi ya Tamasha hilo ambalo halikuwahi kufanyika mkoani humo na imekuwa faraja kwake kama mwakilishi wa wananchi  wa mkoa huo  unaokabiliwa na mauaji kwa walemavu wa ngozi.

Alisema amefurahishwa  kufanyika kwa tamasha hilo mkoani Geita na mikoa mgine kwani ana imani wakazi wa mkoa huo watahamasika  kuacha mauaji ya Watanzania wasio na hatia ambao ni walemavu wa ngozi na vikongwe ambayo yanaendelea. Mbunge huyo anaelezea furaha yake, ana imani wananchi wa mkoa wa Geita watafurahi kwa sababu mkoa huo umesuswa kwa kuwapelekea matamasha ya namna hiyo na kusikia yanafanyika katika mikoa mingine kama Dar es Salaam na Mwanza.

"Nimefurahi sana Msama kulileta Tamasha hili litakalopiga vita mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi, nina imani wananchi wataweza kuelimika kwa njia moja au nyingine, baada ya hapo inawezekana kabisa likaweza kubadilisha fikra na mtizamo juu ya suala hili na kupunguza kabisa mauaji haya," anasema Lolensia.

Alieleza kuwa limekuwa jambo la bahati kwa mkoa huo kufikiwa na tamasha hilo ambalo lina mafanikio makubwa katika kutimiza malengo yanayokusudiwa hivyo anaamini kilichokusudiwa kwa Geita kitafanikiwa kwa kiasi kikubwa. "Tunawakaribisha sana na nichukue nafasi ya pekee kumpongeza Msama kwa uamuzi wake wa kutuletea tamasha hili tunatarajia kupata mambo makubwa pia nina imani wanageita watafurahia mno kwasababu wanapenda mambo hayo ya muziki hasa huu wa Injili," alisema Lolensia.

Aidha alifafanua kuwa ana uhakika wananchi watalifurahia na watafika kwa wingi na hata wale wa pembezoni mwa mji huo kwani kote huko wameathirika na mauaji. Lolensia alisema kuwa Msama sio kampuni ngeni masikioni mwake anaifahamu muda mrefu huku akisisitiza kuwa amewahi kuiandikia barua ya kuomba sapoti  kwa ajili ya watu wake wa jimbo, hivyo anafurahi kuwa Msama ameamua kwenda mwenyewe.

"Kama kampuni ya Msama imeamua kuja Geita tunafurahi maana ataweza kutoa sapoti kwa njia hii maana wahitaji wako wengi ukizingatia eneo lenyewe linashughuli nyingi za kiuchumi" alisema.

Alizitaja baadhi ya shughuli hizo ni  pamoja na uchimbaji wa madini na kwamba watu wengi wanaingia na kutoka hivyo inasababisha wingi na watoto wanazaliwa kwa wingi ambako wazazi wao wanajishughulisha na shughuli za kiuchimbaji katika maeneo ya mbali na karibu.

Hivyo watoto hao wanakosa matunzo ya wazazi wao na kupelekea kuwa wa mitaani na wengine kujiingiza katika vitendo viovu . Alisema kwa mtazamo aliokuja nao Mwenyekiti wa Kamati Alex Msama ambaye pia  Mkurugenzi wa Msama Promotions  wa kusaidia jamii ya Geita anamuunga mkono ili aweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Mbunge huyo wa CCM, alisema pengine kufanyika kila mwaka kwa tamasha hilo huenda huo ujumbe utaisaidia jamii kubwa hasa ile ilioingiwa na imani potofu ya kuuwa walemavu wa ngozi  pamoja na vikongwe. 

"Tunaomba kama Msama Promotions wameanza safari hii, basi isiwe mwisho iwe ni mwanzo kwa nia ya kuendeleza jitihada za kuelimisha jamii kadri tunavyopeleka ujumbe ndivyo itakavyowafikia wengi ukizingatia mkoa wetu unachangamoto nyingi." alisema