Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
WILAYA ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi inayotokana na watu waliopata hati kukiuka taratibu za upatikanaji wa hati hizo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokutana na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, amesema kuwa serikali imejipanga katika kutatua migogoro ya ardhi nchi nzima kutokana na kuweka kanda nane zitazofanya kazi ya kutoa hati za viwanja ili kuondokana na migogoro hiyo.
Amesema matatizo mengi ya migogoro ya ardhi iliopo kinondoni inatokana na udanganyifu wa kisheria kwa watu kumiliki ardhi pasipo kuwa na uhalali.
Aidha amesema wananchi wote ambao waligongana wawili katika kiwanja kimoja ambacho wameshalipia watapewa haki yao kutokana na serikali haiko tayari kuona watu wake wanadhulumiwa.
''Ninaahidi kushughulikia matatizo ya ardhi kwa nguvu zote, na wananchi wanatakiwa kuwa wakweli katika utoaji wa taarifa zinazohusiana na viwanja au upatikanaji wa hati''amesema Lukuvi.
Amesema baadhi ya wawekezaji na watendaji wamekuwa wakifanya udanganyifu wa hati za umiliki ardhi na kusababisha migogoro ya adhi kwa wananchi wenye haki za ardhi hiyo.
Waziri Lukuvi amesema kuwa migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na Wananchi inatakiwa kuangaliwa kwa umakini kutokana na unyeti wa chombo cha jeshi na maeneo yao yaliwekwa kwa mkakati maalumu wa usalama wa nchi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,William Lukuvi akizungumza na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyotembelea wizara hiyo kupata taarifa mbalimbali za ardhi iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabura.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,William Lukuvi akionyesha Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira mfumo wa huduma kwa wateja jinsi wanavyoshughulikia matatizo ya ardhi.
Sehemu ya wananchi waliofika Wizara ya wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakipata huduma mbalimbali Wizarani hapo leo jijini Dar e Salaam.Picha na Emmanuel Massaka wa Globu ya jamii.