Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati Dk. Juliana Pallangyo (pichani) akifungua mkutano unaoshirikisha wakurugenzi wa mashirika ya umeme katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika zinazoshirikiana katika biashara ya umeme.
Sehemu ya watendaji na wakurugenzi wa mashirika ya umeme katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika zinazoshirikiana katika biashara ya umeme, wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo (hayupo pichani).
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kulia) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Mhandisi Decklan Mhaiki (kushoto) wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na mwenyekiti wa kamati ya nchi za kusini mwa Afrika zinazoshirikiana katika biashara ya umeme, Josh Chifamba (hayupo pichani)
Mwenyekiti wa kamati ya nchi za kusini mwa Afrika zinazoshirikiana katika biashara ya umeme, Josh Chifamba (kulia) akimkabidhi zawadi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo (kushoto) aliyekuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo (aliyekaa mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watendaji na wakurugenzi wa mashirika ya umeme katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika zinazoshirikiana katika biashara ya umeme, mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk Jualiana Pallangyo amewataka wawekezaji binafsi nchini kujitokeza kwa wingi na kuwekeza katika uzalishaji na uuzaji wa nishati ya umeme nchini ili iweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Dk. Pallangyo alisema hayo kwenye mkutano unaokutanisha wakurugenzi wa mashirika ya umeme katika nchi zilizopo kusini mwa Afrika zinazoshirikiana katika biashara ya umeme. Nchi hizo ni pamoja na Bostwana, Msumbiji, Afrika ya Kusini, Lesotho, Namibia, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Swaziland, Zambia na Zimbabwe. Lengo la mkutano huo wa siku moja lilikuwa ni kujadili changamoto zinazozikumba nchi wanachama katika uzalishaji na uuzaji wa umeme ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu.
Aliongeza kuwa wawekezaji binafsi wanaweza kuzalisha umeme kupitia vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwa ni pamoja na maporomoko madogo ya maji, upepo, bayomasi na jua kutokana na uwezo wao.
Akielezea fursa za uwekezaji nchini, Dk. Pallangyo alisema kuwa wawekezaji wanaweza kuwekeza kupitia ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa umeme, uendelezaji wa miradi ya umeme unaotokana na maporomoko madogo ya maji na vyanzo vingine ikiwa ni pamoja na jotoardhi, upepo na uanzishwaji wa viwanda vidogo kwa ajili ya utengenezaji wa vifaa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umeme.
Dk. Pallangyo aliongeza kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya umeme umeongezeka kila mwaka na kusisitiza kuwa serikali bado inaendelea na mikakati ya kuwawezesha wawekezaji binafsi katika uzalishaji ya umeme nchini.
Aliongeza kuwa serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na sera na sheria mbalimbali zinazotumika kama mwongozo na kutaja kuwa ni pamoja na sheria ya umeme ya mwaka 2008, sera ya nishati ya mwaka 2003 ambayo inahamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya umeme.
Alitaja sheria nyingine kuwa ni pamoja na ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ya mwaka 2001, sheria ya Wakala wa Nishaji Vijijini (REA) ya mwaka 2005.
Akielezea mikakati ya serikali katika upatikanaji wa nishati ya uhakika, Dk. Pallangyo alisema kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia 75 ya wananchi wote hasa waishio vijijini wanapata nishati ya umeme ambayo ni ya uhakika.
"Tunatarajia kuzalisha hadi megawati 10,000 za umeme ambao utachochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia viwanda na hivyo nchi kutoka katika kundi la nchi masikini duniani na kuwa katika kundi la nchi zenye kipato cha kati duniani," alisisitiza Dk. Pallangyo.
Akielezea hali ya upatikanaji wa umeme nchini, Dk. Pallangyo alisema kuwa umeme unaozalishwa ni megawati 1461.69 huku mahitaji halisi yakiwa ni megawati 1026.
Umoja wa nchi zinazoshirikiana katika sekta ya umeme kusini mwa Afrika (Southern African Power Pool; SAPP) ulianzishwa Agosti mwaka 1995 katika Mkutano wa Umoja wa Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) ambapo walisaini makubaliano kwa ajili ya kushirikiana katika uzalishaji na biashara ya umeme wa pamoja.