Thursday, December 03, 2015

WAZIRI MKUU AVAMIA TENA BANDARINI NA TRL,AKUTA MAKONTENA 2431 YEMETOKA BILA KULIPIWA KODI.



WAZIRI MKUU AVAMIA TENA BANDARINI NA TRL,AKUTA MAKONTENA 2431 YEMETOKA BILA KULIPIWA KODI.
  Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akikagua bandari ya Dar es salaam  Desemba 3, 2015 ambako alikwenda kupata ukweli kuhusu makontena 2,431 yaliyopitia kwenye bandari hiyo bila kulipiwa kodi ya serikali.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mfumo wa kukagua makontena bandarini kwa kutumia scaner huku akipata maelzo kutoka kwa Ofisa wa forodha, January Shauri wakati alipotembelea bandari ya Dar es salaam Desemba 3, 2015  kutaka kujua ukweli wa tuhuma za makontena 2431 yaliyopita bandarini hapo bila kulipiwa kodi ya serikali.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu utoaji bili za kulipia kodi za serikali kwa watumiaji wa bandari ya Dar es salaam kutoka kwa ofisa mwandamizi wa masuala ya fedha , Bw. Sartho Mbuya wakati alipotembelea bandari hiyo  Desemba 3, 2015 kutaka kujua ukweli wa tuhuma za makontena 2431 yaliyopita bandarini hapo bila kulipiwa kodi za serikali. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimwonyesha Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es salaam, Bw. Abel Mhanga (kulia) orodha ya makontena 2,431 yaliyopitia kwenye banda ya Dar es salaam bila kulipiwa kodi wakati alipofanya ziara kwenye bandari hiyo Desemba ,3, 2015. 
 Waziri Mkuu,  Kassim Majliwa  akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini TRL wakati alipotembelea stesheni ya Dar es salaam kukagua uendeshaji wa Shirika hilo Desemba 3, 2015. 
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akitembelea steheni ya reli ya Dar es salaam Desemba 3, 2015.


WAZIRI MKUU ATINGA TENA BANDARINI NA TRL
*Akuta makontena 2,431 yametoka bila kulipiwa ushuru
*Ataka majina yaletwe ofisini leo saa 11 jioni
*Atoa wiki wiki moja kwa mfumo wa malipo kubadilishwa
*Akagua mabehewa, awaweka kiporo TRL

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara nyingine ya kushtukiza bandarini na kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.

Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na AZAM.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10 tu ambao wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo. "Mmeamua kuwasimamisha kazi watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha Serikali mapato namna hii," alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Bw. Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia amempa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment).

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 3, 2015), wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa mizigo unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ben Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha scanner, inapobainika taarifa kama hiyo inapaswa itumwe kwa wenye ICDs ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena ili kuhakikisha mali zilizomo ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Shirika la Reli (TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.

Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha sh. bilioni 13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo. "Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha kibiashara lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe," alisema.

"Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh. bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala ya kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika," alihoji bila kupata majibu.

Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia Julai – Novemba 2014.

Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.

"Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam," alisema.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
ALHAMISI, DESEMBA 3, 2015.