Sehemu inayoendelea kufukiwa hapo Mtoni Marine ambayo itatumika hapo baadae kwa ajili ya eneo maalum litakalotoa fursa kwa Wananchi kupata mapumziko.{ Public Beach }.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis Nassor akimueleza Balozi Seif hatua zinazochukuliwa na Taasisi yake katika kuona taratibu za uwekezaji zinachukuliwa kwa wanaowekeza vitege uchumi vyao Nchini.
Balozi Seif akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa Group Bwana Said Salim wakitembelea kuona mradi wa Ujenzi wa Majengo Mapya ya Hoteli ya Mtoni Marine ambayo iko chini ya Kampuni hiyo kwa hivi sasa.
MRADI mkubwa wa Kimataifa wa ujenzi wa kisiwa cha Kitalii ambacho kitatengenezwa kwa mfumo wa ufukiaji Bahari umeanza rasmi katika eneo la Hoteli ya Utalii iliyopo Mtoni Marine kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar.
Hata hivyo gharama kamili za Mradi huo bado hazijafahamika wakati utakapokamilika rasmi ujenzi wake hapo baadaye.
Mradi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Kizalendo ya Baghresa Group utahusisha ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ghorofa Tano ya Daraja la Tano { Five Star + }, utengenezaji wa eneo la wazi la mapumziko { Public Beach } pamoja na kutengeneza Kisiwa cha Mji mpya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alishuhudia harakati za ujazaji wa mchanga katika eneo linalofukiwa ambazo hufanywa kwa utaalamu wa hali ya juu.
Mhandisi wa Mradi huo Bwana Ahmed Shamsi alimueleza Balozi Seif kwamba chombo maalum kinachotumika kwa kazi ya uchimbaji wa mchanga Baharini kina uwezo wa kunyonya na kusafirisha mchanga kutoka ndani ya Bahari sambamba na kukata Majabali.
Mhandisi Shamsi alisema kazi hiyo inafanyika kwa saa 12 kila siku ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba uchimbaji huo wa mchanga unaokwenda zaidi ya mita 15 chini ya Bahari unafikia Tani 600 za mchanga kwa saa Moja.
Alifahamisha kwamba harakati za uchimbaji na kufukia mchanga katika eneo hilo zilizoanza Mwezi uliopita wa Novemba zinatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka ujao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa Group Bwana Said Salim Baghresa alisema kwamba ujenzi wa mradi huo muhimu kwa uchumi wa Nchi utasaidia mapato ya Taifa pamoja na kutoa ajira kubwa kwa vijana Wazalendo hapa Nchini.
Bwana Baghresa alisema mfumo wa ufukiaji Bahari kwa ajili ya kuanzisha miradi ya Kiuchumi ni mfumo unaotumiwa na Mataifa mbali mbali Duniani ambapo kwa Afrika mradi kama tayari umeanza kutumiwa katika Kisiwa cha Seycheles.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Baghresa Group kwa uamuzi uliochukuwa wa kuanzisha mradi huo mkubwa wa Kimataifa.
Balozi Seif alieleza kwamba kukamilika kwa mradi huo mkubwa ambao umeshazoeleka katika Mataifa yaliyoendelea utasaidia kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla Kiutalii Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Baghresa Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada unaohitajika katika kuona mradi huo unafikia malengo uliojipangia.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamui wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/12/2015.