SERIKALI imekuwa ikijitahidi kuchukua hatua mbalimbali kuboresha elimu nchini na kuondoa kero mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo kwa ngazi zote, kama vile chekekechea, msingi na sekondari.
Miongoni mwa hatua hizo ni kutolewa kwa Waraka wa Elimu Namba 5 wa mwaka 2015, ambao umefuta ada kwa elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne kwa shule za umma na michango yote katika elimu ya msingi.
Kamishna wa Elimu, Profesa Eustela Bhalalusesa, anafafanua kuwa mwongozo wa elimu msingi bila malipo, unaandaliwa na utatumwa kwa wamiliki wa shule ifikapo au kabla ya Desemba 15 mwaka huu.
Kamishna huyo anasema serikali imeamua kutoa elimu pasipo malipo kwa elimu ya msingi kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne kuanzia mwakani. Azma hii ya serikali ni kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 yenye lengo la kuhakikisha kwamba watoto wote wa Tanzania, wanapata elimu bila kikwazo chochote, ikiwemo ada au malipo.
Katika kutekeleza maamuzi hayo, ada zote zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya kidato cha kwanza hadi cha nne zimefutwa. Pia Waraka wa Elimu Namba 8 wa mwaka 2011 kuhusu michango shuleni, nao umefutwa.
Tunaunga mkono hatua hiyo kubwa ya serikali, kwani italeta manufaa mengi kwa wazazi na watoto. Ni dhahiri hatua hiyo itaondoa kero ya michango mingi, ambayo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanatozwa kwa sasa.
Kwa mfano, shule moja ya sekondari huko Shinyanga imekuwa ikitoza kila mwanafunzi anayeanza kidato cha kwanza michango mbalimbali, ambayo jumla yake ni zaidi ya 100,000.
Michango hiyo ni pamoja na ada kwa mwaka Sh 20,000, fagio Sh 5,000, jembe Sh 5,000, ndoo Sh 10,000, bunda la karatasi nyeupe Sh 10,000, dawati 20,000, kiti Sh 15,000, uzio Sh 20,000, tuisheni Sh 500 kwa kila siku kwa kila mwanafunzi.
Shule hiyo ina wanafunzi 200 wa kidato cha kwanza na kila mwaka unapoanza, wanafunzi wapya wanalipa pia malipo hayo. Aidha, katika gazeti letu la jana, tuliripoti kuhusu michango iliyopo katika shule ya msingi Kizwite Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Huko wazazi wa eneo hilo, wameanza kutozwa fedha nyingi kwa ajili ya kuandikisha watoto watakaoanza darasa la kwanza mwakani, ikiwemo kutakiwa kuchangia Sh 19,000 kwa ajili ya ujenzi wa choo kipya.
Kwa hakika, ni kosa kubwa kuendelea kutoza wazazi michango hiyo kwa watoto wao wa shule za msingi na sekondari, wakati tayari serikali imetangaza kuwa itatoa elimu ya bure hadi kidato cha nne kuanzia Januari.
Na tukumbuke kuwa mwezi ujao umekaribia! Tunaomba kama shule zina ukosefu wa miundombinu, wanaotakiwa kubanwa ni wazazi na halmashauri, badala ya kuchangisha watoto. Ni wajibu wa wazazi na halmashauri, kuzipatia haraka shule mahitaji.
Jambo lingine ni maofisa elimu na kamati za shule, kuanzia sasa wafuatilie utekelezaji wa agizo la Serikali na kuhakikisha wazazi hawachangishwi tena michango mbalimbali. Iwe ni marufuku kuanzia sasa wazazi kulipa ada wala kutozwa michango yoyote ile.