Tuesday, December 08, 2015

TGDC NA MKAKATI WA UZALISHAJI WA UMEME KUPITIA JOTOARDHI



TGDC NA MKAKATI WA UZALISHAJI WA UMEME KUPITIA JOTOARDHI
 Meneja Mkuu Shirika la Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe (kushoto) pamoja na Mtaalamu Mkuu toka Kampuni ya TOSHIBA Bwana Kentaro Kurahara wakiweka saini Mkataba wa wa Maelewano (MOU) wa kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi katika Ofisi za TGDC zilizopo Jijini Dar es Salaam.
 Meneja Mkuu Shirika la Uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe (kushoto) pamoja na Mtaalamu Mkuu toka Kampuni ya TOSHIBA Bwana Kentaro Kurahara wakikabidhiana Mkataba wa Maelewano (MOU) wa kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi katika Ofisi za TGDC zilizopo Jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa ICEIDA, Bwana Engilbert Gudmundsson, wakiweka saini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirkiano wa kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini zilizopo Jijini Dar es Salaam.

Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
KUTOKANA na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme nchini, nishati itokanayo na jotoardhi (Geothermal Energy) imetajwa kuwa ni muhimu katika kuepukana na hasara kubwa na isiyo ya lazima inayotokana na matumizi ya mitambo ya mafuta katika kuzalisha umeme na kuifanya Tanzania kuondokana na tatizo la umeme usiokuwa na uhakika pamoja na kuleta maendeleo nchini.

Ili kuleta Maendeleo haya katika sekta ya nishati, Tanzania hainabudi kugeukia katika vyanzo vingine vya uzalishaji umeme ikiwemo nishati hiyo ambayo kwa kutumia mvuke wa maji yaliyochemshwa na joto la asili lililopo chini ya ardhi, nishati ya umeme inaweza kuzalishwa na kukidhi mahitaji ya nishati ambayo yatasaidia kuwa kiunganishi cha ukuaji wa uchumi nchini. 

Tanzania iko katika ukanda wa Bonde la Ufa (Rift Valley), hivyo kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa hifadhi kubwa ya nishati itokanayo na jotoardhi ambayo inaweza kutumika katika uzalishaji wa umeme na kuinua uchumi wan chi yetu.

Nishati hii itakuwa mkombozi kwa taifa letu hususani kwa mwananchi wa kipato cha chini kwani tunaamini kuwa matumizi ya nishati hiyo yatapelekea kupungua kwa gharama za manunuzi ya umeme na kutokana na ukweli kwamba nishati hiyo pindi ipatakinapo haitarajiwi kuisha.

Unafuu wa umeme utakaozalishwa na jotoardhi unatokana na ukweli kwamba mitambo inayotumika kuzalisha umeme huo kuendeshwa kwa mvuke ambao unatokana na majimoto toka ardhini tofauti na uzalishaji wa umeme uliokuwa unatumika kwa kutumia mitambo yenye kutumia mafuta ambayo gharama yake ilikuwa juu kwa Serikali.

Hapa nchini, kuna viashiria vingi vinaonyesha uwepo wa jotoardhi hasa kwa maeneo ya vijijini ambako umeme sehemu nyingi haujafika, kutokana na hilo sasa Serikali yetu hainabudi kutupia macho katika nishati hii kwa kuhakikisha kwamba wananchi ambao wnaaishi maeneo ambayo nishati hiyo inapatikana wananufaika na umeme huo.


Jotoardhi ina matumizi mengi kwa jamii yetu, mfano majimoto yatokayo ardhini yanaweza kutumika katika kukaushia mazao mfano matumizi ya Vitalu shamba(Green Houses) badala ya kutegemea jua. Mwananchi wa kipato wa chini anaweza kutumia majimoto kukausha mazao yake kwa mfano mpunga, maharage, mahindi, karanga katika ubora ule ule kama wa jua. 

Matumizi mengine ya majimoto ni katika kupasha nyumba joto hasa katika wananchi wale waishio mikoa yenye baridi kali kwa kujenga mabomba ya kupitisha maji ya moto ndani ya nyumba zao.

Shirika la Uendelezaji Nishati ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) imepewa lengo na Serikali la kuhakikisha kuwa inazalisha umeme wa Megawati 200 na kuuingiza katika gridi ya Taifa kufikia mwaka 2020.

Hivi karibuni, TGDC kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (ESMAP) zilifanya warsha ya siku mbili iliyofanyika Jijini Dar es Salaam ambayo iliwakutanisha wadau kutoka Mashirika mbalimbali yanayoshughulikia masuala ya jotoardhi yakiwemo GDC la Kenya, Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), BGR la Ujerumani, ICEIDA la Iceland, Chuo cha Umoja wa Mataifa kinachofundisha nishati ya Jotoardhi (UNU), TNO la Uholanzi pamoja na Shirika la Star Energy la nchini Indonesia ambapo wadau hawa wote wameweza kufanikiwa kuipata nishati hiyo, hivyo watatoa mchango mkubwa kuliwezesha shirika la TGDC kupata mafanikio na hatimaye nishati hiyo kuweza kupatikana.

Katika warsha hiyo, Meneja Mkuu wa Shirika la Uendelezaji nishati ya Jotoardhi (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe alisema kuwa warsha hiyo inalenga kujadili kwa kina njia mbalimbali zilizotumiwa na baadhi ya mashirika hayo hadi kufanikiwa kupata nishati hiyo ikiwemo uanishaji wa huduma tofauti zifanywazo na mashirika hayo katika kulisaidia shirika la TGDC. 

"Matokeo ya warsha hii tuliyoifanya tumeweza kuwasiliana na wenzetu wa Benki ya Dunia (ESMAP) kwa kukusanya wataalam toka taasisi mbalimbali pamoja na Mashirika mbalimbali ambayo yamewahi kufanya kazi hii ya utafutaji wa nishati ya jotoardhi na lengo letu ni kutaka kufahamu njia ambazo wenzetu walizitumia mpaka kufanikiwa ili na sisi tupate kujifunza", alisema Njombe.

Mhandisi Njombe aliongeza kuwa warsha hiyo itawezesha rasilimali chache zilizopo ziweze kutumika ipasavyo katika kuleta matokeo ambayo TGDC inatarajia kuyapata ili kuhakikisha kuwa lengo la upatikanaji wa nishati hiyo linafikiwa.

Sambamba na warsha hiyo, Serikali kupitia TGDC na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la nchini Iceland (ICEIDA), wamesaini Mkataba wa Makubaliano utakaowezesha Tanzania kunufaika na msaada wa kiasi cha Dola za Marekani 1,565,000 kwa ajili ya kupata Mtaalam mwelekezi kufanya tafiti katika maeneo yenye viashiria vya Jotoardhi ikiwemo kuwajengea uwezo Wataalam wetu wa hapa nchini pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya utafiti wa nishati hiyo.

Makubaliano hayo yalifikiwa Jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, kati ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Paul Masanja na Mkurugenzi Mkuu wa ICEIDA, Bwana Engilbert Gudmundsson, huku likishuhudiwa na Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe, Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Uendelezaji wa Nishati Jadidifu, Bwana Edward Ishengoma pamoja na baadhi ya Maafisa kutoka TGDC na Wizara ya Nishati na Madini.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa Mkataba huo, Mhandisi Paul Masanja alisema kuwa, matarajio ya Tanzania ni kuzalisha kiasi cha megawati 200 za umeme unaotokana na nishati ya jotoardhi ifikapo mwaka 2020, ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa, hazina iliyopo kupitia nishati hiyo ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya umeme wa megawati 5,000, kutokana na nishati ya jotoardhi toka ardhini.

Mhandisi Masanja aliongeza kuwa, utayari na ushirikiano unaoonyeshwa na nchi ya Iceland kupitia Shirika la ICEIDA itakuwa kichocheo kikubwa kufikia malengo ya Serikali ya kuwa na nishati ya kutosha ya umeme na kuchochea maendeleo nchini.

"Tuna malengo mengi kupitia nishati hii ya jotoardhi, utafiti ndio njia itakayotufanya kufikia malengo haya, ushirikiano huu ni mwanzo mzuri kwa upande wetu sisi Tanzania, na nafahamu kuwa Iceland mlianzia katika hatua za chini kabisa lakini sasa mko mbali, zoefu wenu katika masuala haya ya nishati hii utatuwezesha kuweza kufika mahali tunapotarajia," alisema Mhandisi Masanja.

Naye, Mkurugenzi wa ICEIDA, Bwana Engilbert Gudmundsson alieleza juu ya umuhimu wa nishati hiyo na unafuu wake wa gharama ikilinganishwa na nishati nyingine na kueleza kuwa, zaidi ya asilimia 25 ya umeme unaozalishwa nchini Iceland unatokana na nishati ya jotoardhi, hivyo Tanzania inaweza kufikia malengo yake ya kupata nishati hiyo kwa kuonyesha juhudi zake ikiwemo kushirikiana na ICEIDA.

"Sisi Ilituchukua kipindi cha miaka 25 kufikia mafanikio tuliyonayo katika nishati ya jotoardhi, hivyo kutokana na uzoefu wetu huu hatunabudi kutoa uzoefu wetu kwa TGDC ili kuhakikisha inafakia malengo," alisema Gudmundsson.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe alishukuru na kuonyesha hali ya utayari wa ICEIDA katika kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia malengo yake ya kuendeleza nishati hiyo, utakaosadia kufanyika kwa tafiti katika maeneo mbalimbali yenye viashiria vya nishati hiyo kama vile maeneo ya Luhoi pamoja na Kibiti Mkoa wa Pwani.

Mhandisi Njombe anabainisha kuwa, kutokana na utafiti utakaofanywa kwa ushirikiano kati ya TGDC na ICEIDA, utawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na halisi ambazo zitafungua njia ya kupata misaada zaidi kutoka katika taasisi na wahisani mbalimbali ambao wamejikita katika masuala nishati hiyo.


Moja ya hatua mbalimbali ambazo zilizofanywa na TGDC mpaka hivi sasa ni kwamba jotoardhi inakuwa chanzo kingine cha uzalishaji umeme nchini na kupitia makubaliano hayo, ICEIDA itawezesha Wataalam wa ndani kutoka TGDC kupata ujuzi na uzoefu utakaowezesha kufanyika kwa tafiti nyingine katika maeneo mengine huko mkoani Mbeya.

Katika hatua nyingine TGDC pamoja na Kampuni ya TOSHIBA ya nchini Japan zimetiliana saini Mkataba wa Maelewano wa kufanya tafiti kwa pamoja zinahusu maeneo yenye viashiria ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi.

Utiaji saini wa mkataba ni hatua nzuri ambayo sasa inaliwezesha Shirika la TGDC kuweza kupata msaada wa kitaalam ambao utaliwezesha shirika hilo kuweza kuchimba ardhini kwa lengo la kupata mvuke utakaoweza kuzalisha umeme.

Akiongea wakati wa tukio la utiaji saini wa Mkataba huo, Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe alisema kuwa kupitia Serikali ya Japan hususani Shirika la Maendeleo Japan (JICA), Kampuni ya TOSHIBA watasaidia kuomba ufadhili wa Serikali yao ili kuweza kuendeleza ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme pamoja na matumizi mengine yanayoendana na nishati hiyo.

"Katika utafiti wa nishati ya jotoardhi tunahitaji watu wenye elimu na uzoefu na ujuzi wa kutosha, miongoni mwa makubaliano ndani ya mkataba huu tuliosaini leo ni wafanyakazi wetu kadhaa kuwapeleka nchini Japan kwenye vyuo vyao ili kuweza kupata mafunzo ya darasani na kutembelea maeneo ambayo Japan wana vituo vya jotoardhi ili wapate ujuzi wa kufanya kazi na Wajapan na kutuletea ujuzi huo hapa nchini", alisema Njombe.

Kupitia ushirikiano huu unaoonyeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania, tuna imani kuwa nchi ya Japan itaendelea kuisadia Tanzania katika kuendeleza nishati ya jotoardhi kwakuwa ni nishati yenye tija katika kutimiza ndoto za Tanzania kwa kuifanya kuwa nchi yenye kipato cha kati kufikia mwaka 2020.

TGDC inatarajia kuanza kuainisha maeneo ya ushirikiano wa pande hizi mbili (TGDC na TOSHIBA) ikiwemo kuyawekea muda wa utekelezaji ambapo mwezi Machi mwakani, Wataalam toka TGDC wataweza kwenda nchini Japan kwa ajili ya kwenda kupata elimu zaidi kuhusu nishati hiyo.

Mtaalamu Mkuu toka Kampuni ya TOSHIBA Bwana Kentaro Kurahara anaeleza kuwa kampuni yao iko tayari kuisaidia Tanzania katika masuala yanayohusu jotoardhi na iko tayari kuomba ufadhili kupitia Serikali ya Japan ikiwemo kuwapa Wataalam wa TGDC elimu ya kutosha inayohusu nishati hiyo ili waweze kuhakikisha kuwa nishati hiyo inapatikana na kuleta maendeleo kwa Tanzania.

"Tunafuraha ya kushirikiana na TGDC katika kufanya tafiti zinazohusu jotoardhi kama mkataba wetu tuliousaini unavyosema, kupitia Serikali ya Japan na Shirika la JICA tutaomba ufadhili kwa ajili ya TGDC ili muweze kuleta wataalam wenu kuja kujifunza Japan pamoja kuwasaidia katika masuala mengine yanayohusu shughuli ya utafutaji wa nishati hii", alisema Kurahara.

TGDC ikiwa kama Shirika Tanzu lililopo chini ya Kampuni ya Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) limepewa lengo na Serikali la kuharakisha upatikanaji wa nishati ya jotoardhi kufikia Megawati 200 mwaka 2020. Kampuni hiyo imesajiliwa Disemba 19, 2013 na kuanza kufanya kazi Julai 2014 huku ikipewa jukumu la kuharakisha uendelezaji wa nishati ya Jotoardhi nchini ambapo mpaka hivi sasa TGDC imegundua Zaidi ya maeneo yenye viashiria vya jotoardhi ambayo yamegawanyika katika Kanda Nne ambazo ni Kanda kaskazini–Ziwa Manyara, Kreta ya Ngorongoro, Natron na Majimoto Mara, Kanda ya Mashariki–Utete (Pwani), Kisaki (Morogoro), Luhoi (Pwani), Kanda ya Magharibi–Ibadakuli (Shinyanga), Mtagata(Kagera), maeneo mengine ni Dodoma, Singida pamoja na Tanga.