Tuesday, December 01, 2015

JAJI MAKURU AFUNGUA MAFUNZO MAALUM YA HUDUMA KWA WATEJA KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA YA TANZANIA.



JAJI MAKURU AFUNGUA MAFUNZO MAALUM YA HUDUMA KWA WATEJA KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA YA TANZANIA.
 Watumishi wa Kada mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria mafunzo ya Huduma kwa wateja ili kuweza kuwajengea ujuzi na ufanisi katika kazi mahakamani.
 Mhe. Jaji Crescencia Makuru, Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma, akifungua rasmi mafunzo maalumu ya Huduma kwa Wateja kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania, leo mkoani Dodoma. 
Mhe. Jaji Crescencia Makuru, Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma, (aliyeketi wa pili toka kushoto), Nurdin Ndimbe, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Mahakama ya Tanzania, (wa pili kulia), Deus Kibamba, Mkurugenzi wa TCIB, (wa kwanza kulia), Simon Berege, Mwenyekiti wa MISA-Tanzania, (wa kwanza kushoto), katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kada mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania washiriki wa mafunzo ya Huduma kwa Wateja,                Mkoani Dodoma.  
                                                                                                                                                                   
MAFUNZO maalumu ya siku mbili yahusuyo huduma kwa wateja na haki ya kupata taarifa kwa watumishi wa Mahakama, yamemalizika leo katika hoteli ya St.Gaspar mjini Dodoma.

Akifungua rasmi mafunzo hayo  Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma, Mhe. Crescencia Makuru, amesema moja ya malengo makuu ya mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama kwa kuwapa mbinu na mikakati mbalimbali itakayowasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

"Mahakama ya Tanzania kwa sasa inaendelea na maboresho ya utendaji kazi wake kama sehemu ya kuhakikisha kuwa inatoa huduma iliyo bora na kwa wakati", Jaji Makuru amebainisha.

Mwaka 2014 Mahakama ya Tanzania kama moja ya Taasisi ya Serikali ilifanyiwa tathmini kuhusu utoaji wa haduma zake hasa katika nyanja ya upatikani na utoaji wa taarifa kwa Umma iliyoendeshwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, (Media Institute of Southern Africa-MISA). 

Katika tathmini ile, Mahakama ilikuwa ya mwisho na ilizawadiwa kufuli la dhahabu kama alama ya kuonyesha kuwa taasisi hii ni moja kati ya zilizojifunga sana kutoa taarifa kwa wananchi. Moja ya maeneo yaliyoonekana na udhaifu ni namna masijala za Mahakama zinavyopokea na kutunza nyaraka na hata wanavyowahudumia wateja kwa ujumla.

Mafunzo hayo endelevu yamelenga kuwafundisha makarani na watumishi wa kada mbalimbali nini maana ya uhuru wa Habari na habari ni Nini?, Huduma kwa wateja na ujuzi wa mawasiliano kwa watumishi wa Umma , Njia mbalimbali za upatikanaji wa taarifa katika Taasisi za Umma na Sheria ya utoaji wa  habari katika Mahakama.

Mafunzo haya yameandaliwa na kufadhiliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) pamoja na Taasisi ya Friedrick Ebert Stiftung (FES) ofisi ya Tanzania.