Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akihutubia wakati wa uzinduzi rasmi wa kujiunga kwa Benki ya Walimu katika Soko la Mitaji Dar es Salaam mwishoni mwa wiki
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amekipongeza chama cha Walimu Tanzania kwa kujiorodhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kupitia benki ya chama hicho kwa ajili ya kuendeleza mtaji wake na kukuza kipato cha wanachama wake.
Waziri Mkuu alitoa pongezi hizo alipokuwa akizindua rasmi hatua ya benki hiyo, Mwalimu Commercial Bank (MCB) kujiorodhesha DSE mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam tayari kwa kuanza kuuza hisa zake.
"Soko la hisa ni njia mpya ya kuwakwamua walimu kiuchumi na kuzidi kujiendeleza kimaisha," alisema.
Alisema serikali ya awamu ya tano imeweka kipaumbele katika kuendeleza elimu, ikiwamo kuboresha maslahi ya watendaji wake na kwamba hatua iliyofikiwa na Chama hicho ni chachu ya kufikia malengo hayo ya maendeleo.
"Chama kimepiga hatua kubwa ya kuanzisha benki kwa kushirikiana na watalaamu mbalimbali, wanachama kuhamasika kuchagia fedha kwa kununua hisa za benki na hatimae leo kujiunga na soko hili,"alisema Waziri Mkuu.
Pia aliipongeza Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Masoko na Mitaji kwa kutoa mwongozo hadi benki ya chama hicho kufikia hatua ya kuuza hisa kwa waalimu mwezi March 2015.
"Mimi ni mwalimu na kwa kweli walimu tupo wengi nchini, majengo ya chama cha walimu yaliyopo mikoani pia yatumike katika kufungua matawi ya benki ili kuwafikia walimu wote na wadau mbalimbali," alisema Bw. Majaliwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Benki ya Walimu, Bw. Herman Kessy alisema mafanikio ya benki yaliyopatikana yanatokana na wanahisa wakiwemo walimu wote wa Tanzania, Mfuko wa Watumishi wa Serikali (PSPF), Mfuko wa Afya ya Jamii (NHIF) pamoja na wanahisa wengine wote wa benki.
"Tumekusanya mtaji wa Tshs Bilioni 31 na matarajio yalikuwa kupata bilioni 25," alisema na kufafanua kuwa walikusanya zaidi ya matarajio yaliyokuwepo kupitia wanahisa 235,494.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bw. Yahaya Msulwa alisema maandalizi ya awali ya kuanzisha benki hiyo yamefikia hatua nzuri kwani wamepata leseni kutoka benki kuu ya Tanzania na wanatarajia itafunguliwa rasmi Mwezi Mei 2016.
"Maandalizi meninge ni pamoja na utengenezaji wa majengo, ununuzi wa mtambo wa kompyuta wa kuendeshea benki (Core Banking System) pamoja na ajira kwa wafanyakazi," alisema.
Benki hiyo inatarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kutatua matatizo ya walimu na watumishi wa serikali na umma kwa ujumla.