Sunday, November 29, 2015

Tutakomesha biashara haramu ya magogo, maliasili—Serikali



Tutakomesha biashara haramu ya magogo, maliasili—Serikali
Serikali imesema vita dhidi ya biashara haramu ya magogo itazidishwa ili kuokoa rasilimali muhimu za misitu Tanzania. Biashara hiyo ni kinyume na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 inayozuia kusafirisha magogo yasiyoongezwa thamani kwenda nje ya nchi. 
 Akiongea na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru alisema kamwe biashara hiyo haitakubalika kuendelezwa na watu wasio waaminifu kwa taifa lao. 
 "Tutapambana nao mpaka tabia hii ikome," alisema wakati wa kukamatwa kwa kontena 31 zilizokuwa na magogo ya miti aina ya mitiki katika bandari ya Dar es Salaam. 
 Aliwataka raia wema kutoa taarifa pale wanaposikia uhalifu kama huo ukitendeka hapa nchini na kusisitiza kuwa vyombo vinavyohusika viko makini kuzuia tabia hiyo. 
 Magogo hayo yenye thamani ya Tshs Milioni 300 yalikamatwa baada ya wizara hiyo kupatiwa habari kuwa kuna makontena yenye magogo bandarini yanasafirishwa kwenda nje ya nchi. Alisema kontena hizo za futi 40 zilijazwa magogo yaliyodaiwa kutoka nchini Zambia. 
 Akifafanua zaidi alisema pamoja na kuwepo kwa madai kuwa mzigo huo unatoka Zambia hapakuwepo nyaraka halali inayoonyesha umetoka kweli nchi hiyo jirani. 
 Naibu Balozi wa Zambia nchini, Bi. Elizabeth Phiri alikuwepo bandarini hapo kushuhudia tukio hilo. Nakala ya nyaraka zilizopatikana kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) kitengo cha bandari ya Dar es Salaam zinaonyesha kuwa magogo hayo yalisafirishwa kutoka Zambia. Hata hivyo balozi huyo mdogo alipoangalia nyaraka hizo na kuomba kupatiwa nakala halisi aziangalie aliambiwa zimebaki mpakani, Tunduma. 
 Maafisa wa TRA waliokuwepo katika eneo la tukio walitakiwa kufuatilia nyaraka halali za kuruhusu magogo kuingia Tanzania. 
 "Ikithibitika vinginevyo ni lazima mtandao huu utokomezwe," alisema Dkt. Meru. 
 Alisema kama hakutakuwa na nyaraka halali, serikali kupitia wizara hiyo itawashughulikia kisheria maofisa walioshiriki kufanya uharibifu huo. 
 "Ni lazima watanzania watambue kuwa hizi ni rasirimali za nchi, serikali haitakubali zifanyiwe uharibifu na baadhi ya watu wachache," alisema. 
 Alisema watashirikiana na vyombo vyote ikiwemo TRA, uhamiaji na vingine kukomesha tabia hizo. Balozi Phiri alisema panatakiwa kufanyika uchunguzi ili kujua yalikotoka magogo hayo. 
 "Siwezi kusema lolote juu ya uhalali wa magogo haya kutoka nchini kwangu, tusubiri uchunguzi," alisema na kuongeza kuwa hata Zambia hairuhusu biashara ya magogo. Alisema vita hivyo vinapaswa kupiganwa kwa ushirikiano wa nchi majirani.
Naibu Balozi wa Zambia nchini, Bi. Elizabeth Phiri (katikati) akielezea jambo waandishi wa habari na maafisa wengine katika bandari ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ambapo kontena 31 zilizojaa magogo ya miti aina ya mitiki yalikamatwa.  Awali ilielezwa kuwa mzigo huo ulitoka nchini Zambia; uchunguzi unaendelea kuthibitisha hilo.  Kushoto ni Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru.