Thursday, October 15, 2015

Maduka ya Uchumi Supermarket yafungwa Tanzania na Uganda




Maduka ya Uchumi Supermarket yafungwa Tanzania na Uganda
Uongozi wa Uchumi Supermarket umetangaza kufunga shughuli zake katika maduka yake yaliyopo Tanzania na Uganda ili kutoa nafasi ya kuzuia mtikisiko wa kifedha unaoikumba kampuni hiyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Uchumi, Dk Julius Kipng'etich, amesema Bodi imeamua kufunga vitengo vya kikanda ili kuimarisha shughuli zake nchini Kenya baada ya kupata hasara katika maduka yake ya Uganda na Tanzania.

"Maduka yetu ya Uganda na Tanzania huchangia asilimia 25 tu ya gharama za uendeshaji. Matawi hayo mawili hayajapata faida yoyote kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita jambo linaloyumbisha shughuli zetu," amesema Dk Julius

"Tuna uhakika kwamba tunaweza kuigeuza Uchumi kwa kulenga asilimia 95 ya biashara ambazo zinaleta fedha kwa wanahisa ambao wana matumaini kwamba tutafanikisha hili ndani ya muda mfupi," ameongeza Dk Kipng'etich.

Kwa upande wa Tanzania, juzi wafanyakazi zaidi ya 400 waligoma kwa kujifungia ndani ya ofisi zao kwa zaidi ya saa 20 wakitaka kujua hatma yao kwenye makao makuu ya duka hilo yaliyopo katika jengo la Quality Center jijini Dar es salaam.