Sunday, September 20, 2015

WANASIASA WALALAMIKIWA KUSAHAU WAZEE KATIKA SERA ZAO



WANASIASA WALALAMIKIWA KUSAHAU WAZEE KATIKA SERA ZAO


Chama cha Wastaafu na Wazee Mkoa wa Mtwara (Chawamu) kimelalamikia wanasiasa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi kuwasahau wazee katika sera zao.



Katibu wa chama hicho, Wilbard Nandonde, alisema chama kinashangazwa na baadhi ya wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani kutoongelea kuhusu mustakabali wa changamoto zinazowakabili wazee na badala yake kujikita kutoa ahadi katika nyanja nyingine.

Alisema waliamua kusambaza makaratasi katika vyama mbalimbali vya siasa na ofisi za serikali, ambazo zinaelezea changamoto hizo zilizoshindwa kutatuliwa kwa kipindi kirefu.

Tumegawa katika ofisi zote za vyama na baadhi ya wagombea tumewapatia..sasa hayo mambo yako mengi lakini sisi tunaomba tu kwamba wazee wasitusahau katika kunadi sera zao au katika manifesto yao wawe wanatutaja sisi wazee watatufanyia nini.. alisema.

Alisema yapo mapendekezo mengi ya wazee ambayo serikali bado haijayafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kutopitishwa kwa sera ya wazee ya mwaka 2003 kuwa sheria ambayo kwa kiasi kikubwa ingeweza kuwalinda.

Angalia toka 2013 mpaka leo ni karibu miaka 12 lakini hii sera bado haijatungiwa sheria...mambo mengine ya manyanyaso labda mtu anakutukana, kama ingekuwa sheria sisi wenyewe tungechukua hatua.

Mtu anayekutukana unamkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, lakini kwa sababu ni sera inaonekana haina mguvu yoyote.. aliongeza.

Aidha, alisema suala la kupata bure huduma za matibabu halitekelezwi na kuzitaka halmashauri zote kuandaa vitambulisho vya wazee kwa ajili ya kutambulika na kupatiwa matibabu bila kulipia gharama yoyote.

Alitoa wito kwa serikali kukomesha vitendo vya mauaji ya wazee ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikitokea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, vinatokana na baadhi ya watu kuwa na imani potofu za kishirikina.

Mwanachama wa chama hicho, Erntrudis Mpokwa, aliitaka manispaa ya Mtwara Mikindani, kutoa msamaha wa kodi za majengo kwa wazee wastaafu wa manispaa hiyo ambao uwezo wao wa kipato ni mdogo na hata nguvu ya kutafuta kipato sio kubwa kiasi cha kumudu gharama ya kulipa Sh. 20,000 inayotozwa kwa mwaka.

Mchina Nnamba, alisema kodi inayotozwa na manispaa hiyo sio ya nyumba isipokuwa ni ya mtaa kwa sababu viwango vinatozwa kutokana na hadhi ya nyumba ni tofauti.

ìSasa matokeo yake hawatozi kodi ya thamani ya nyumba, ila watoza kodi ya mtaa ambayo haipo..mimi jana (juzi) nilipewa hiyo barua nikawaambia haya madai yenu ni ya mtaa na sio ya nyumba, nyumba yenye thamani hii mimi sina kwanza uiwahi kufika ukaiona hiyo nyumba?..hilo ni jambo ambalo wazee wamelalamika mara nyingi..î alisema.

Chama hicho kimejipanga kuadhimisha siku ya wazee duniani katika wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa itakayofanyika Oktoba mosi, mwaka huu, ambapo kitaifa itaadhimishwa mkoani Kigoma.