Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amepokea malalamiko na kero zaidi ya 360 kutoka kwa baadhi ya wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa wizara kusikiliza na kutatua kero zinazohusiana na migogoro ya ardhi.
Aidha, Lukuvi amemteua Paulo Masoyi kuwa Ofisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Temeke, kufuatia aliyekuwa akishika nafasi hiyo Godian Muhindi kuondolewa katika nafasi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kupokea malalamiko hayo, Lukuvi alisema utafiti ukishafanyika hadi kufikia Novemba, mwaka huu wakazi hao watapatiwa hati miliki, kulipwa fidia, kufanyiwa upimaji pamoja na kuwaondoa wavamizi katika maeneo ya watu na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alisema migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikisababishwa na baaadhi ya watendaji katika wizara hiyo wasio waaminifu na kushindwa kuwajibika, jambo ambalo limeendelea kuleta kero kubwa kwa wananchi.
"Hati miliki haina haja ya kutolewa baada ya miezi mitatu au mwaka mmoja iwapo mtu ana vigezo vyote vya kupewa hati, mfumo tuliouanzisha wa kieletroniki utasaidia sana kutoa taarifa kuhusu viwanja vilivyopimwa kupitia simu za mkononi ili kuboresha matumizi sahihi ya ardhi," alisema Lukuvi.
Mmoja wa wakazi wa Kitunda, Novatus Nyiratu, alisema wakazi wapatao 6,000 katika eneo hilo wana malalamiko yao kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi ikiwamo kutolipwa fidia.
Lukuvi alisema malalamiko hayo pamoja na mengine amekwishayapokea katika sehemu mbalimbali nchini na tayari mikoa ya Mbeya na Mwanza imeanza kushughulikia malamiko hayo ili kuyapatia ufumbuzi na kwa asilimia 70 yametatuliwa.
Alisema ili kushughulikia migogoro ya ardhi, wizara itaanzisha madawati ya kusikiliza kero katika kila halmashauri nchini.
CHANZO: NIPASHE