Friday, September 25, 2015

JK: MWENYE TATIZO NA MUSWADA WA HABARI ALETE MAONI SERIKALINI BADALA YA KUKAA NA KULALAMIKA


JK: MWENYE TATIZO NA MUSWADA WA HABARI ALETE MAONI SERIKALINI BADALA YA KUKAA NA KULALAMIKA
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
·         Aunga mkono asilimia 100 staili ya Kampeni ya Magufuli
·         Asema Tanzania inahitaji mawazo mapya ili iweze kusonga mbele
·         Atamani muda wake wa kuongoza Tanzania kumalizika haraka zaidi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya  Mrisho Kikwete amesema kuwa kama wapo watu binafsi ama taasisi yoyote mahali popote wenye matatizo na Sheria ya Takwimu mpya ama Muswada wa Habari nchini basi wawasilishe mapendekezo yake Serikalini ili yafanyiwe kazi badala ya kukaa na kulalamika pembeni ama kwenye vyombo vya habari.

Rais Kikwete pia amesema kuwa ni jambo zuri na jema kuwa Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM anaelezea fikra na matumaini ya kuleta  mabadiliko makubwa zaidi katika uendeshaji wa Tanzania tofauti na uendeshaji huo ulivyo chini ya uongozi wake.

Vile vile, Rais Kikwete amesema kuwa anatamani muda uende kwa kasi zaidi ili aweze kukabidhi madaraka ya kuongoza Tanzania kwa Rais wa Tano,  ili yeye apate muda wa kumpumzika baada ya kazi ngumu ya miaka 10 ambayo ameilezea kama mzigo mkubwa.

Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumanne, Septemba 22, 2015 wakati alipozungumza na wafanyakazi wa taasisi nne za Marekani  ambazo kwa namna moja ama nyingine zimefanya kazi na Serikali yake katika miaka 10 ya uongozi wake mjini Washington, D.C., ambako Rais amefanya ziara ya siku mbili ya kikazi.

Rais Kikwete amezungumza na wafanyakazi wa taasisi za National Democratic Institute (NDI) yenye uhusiano na chama cha siasa cha Democratic, International Republican Institute (IRI) yenye uhusiano na chama cha siasa cha Republican, International Foundation for Electoral Systems (IFES) na United States Institute of Peace (USIP) kwenye makao makuu ya NDI.

Wakati wa kipindi cha maswali na majibu na wafanyakazi wa taasisi hizo, Rais Kikwete ameulizwa swali kuhusu madai kuwa Sheria ya Takwimu na Muswada wa Habari inavuruga sifa za kidemokrasia za Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete.

Akijibu swali hilo, Rais Kikwete amesema: "Nimelizungumza hilo huko nyuma na napenda kurudia. Sheria ya Takwimu inahusu tu takwimu rasmi za Serikali na wala si takwimu zote. Pili Sheria hii inatokana na matakwa na taratibu za Umoja wa Mataifa na Sheria yetu imetungwa kwa kutilia maanani matakwa ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa. Kwa nini hili linakuwa tatizo kwa Tanzania pekee ni jambo gumu kueleza."

Kuhusu Muswada wa Sheria ya Habari, Rais Kikwete amesema: "Nimelisema hili huko nyuma lakini inaelekea halijaeleweka. Nilipata kusema pale Dar es Salaam na hata wakati nazungumza na wabunge wa Sweden mjini Stockholm kuwa kama mtu ana tatizo ama maoni na maudhui ya Muswada ule basi ayafikishe Serikali. Tutafanyia kazi. Hakuna tatizo na jambo hili. Ajabu ni kwamba tunachosikia ni malalamiko tu na hakuna yoyote ambaye amefikisha maoni yake kwetu."

Hata hivyo, Rais Kikwete ameongeza: "Jambo muhimu ambalo lazima sote tuelewane hapa ni kwamba Muswada wowote, uwe wa habari ama wa jambo jingine, ni lazima ulinde maslahi ya nchi yetu, yalinde umoja wetu, yalinde utulivu wa nchi yetu na yalinde usalama wa nchi yetu. Haya ni mambo ambayo hatuna haja ya kujadiliana na yoyote kwa sababu nchi zote duniani zinalinda kwa namna hii na zinaendeshwa namna hii."

Rais Kikwete pia ameunga mkono mwenendo wa mgombea urais wa CCM wakati wa kampeni ya Uchaguzi mkuu inayoendelea nchini, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, akisema: "Wamepata kuja watu kwangu… wakaniambia kuwa Mgombea wetu wa CCM anashutumu na kusahihisha Serikali yangu na utendaji wake kwenye mikutano ya kampeni. Niliwaambia  hivi…..analofanya Mgombea wetu ni jambo sahihi na barabara kabisa na lazima afanye hivyo."

Ameongeza Rais Kikwete: "Niliwaambia nchi yetu inahitaji mawazo mapya na mwelekeo mpya ulio tofauti na uongozi wangu. Niliwambia kuwa tuliporuhusu jambo hilo kufanyika, nchi yetu itabakia pale pale ambako nimeifikisha mimi. Haya yatakuwa na makosa makubwa kwa sababu nchi yetu lazima isonge mbele kwa mawazo mapya, kwa uongozi mpya na kwa staili mpya ya uongozi. Na haya ndiyo anayasema Mgombea wetu. 

Vinginevyo ni jambo lisilokuwa na maana kubadilisha uongozi kama hatuko tayari kukubali kuwa kila kiongozi lazima awe na staili yake ya uongozi na namna yake ya kuongoza na kuendesha nchi yetu."
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
24 Septemba, 2015