SIKU mbili baada ya mawaziri watano kushindwa katika kura za maoni ya ubunge ndani ya CCM, waziri mwingine, Gaudentia Kabaka anayeshughulikia Kazi na Ajira, naye amedondoshwa katika jimbo la Tarime Mjini.
Kabaka, kabla ya kujitosa katika siasa za majimbo, alikuwa mbunge wa muda mrefu wa viti maalumu. Aidha, katika kura hizo zilizofanyika kote nchini, zimewaacha katika hali mbaya wabunge wanne, baada ya kushindwa katika kura za maoni majimboni mwao.
Hao ni Nyambari Nyangwine, Gaudence Kayombo, John Lwanji na Salome Mwambu.
Matokeo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini ambako Nyangwine ameanguka, yamethibitishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu Wazazi Wilaya ya Tarime, Mathias Lugola aliyetangaza rasmi matokeo ya majimbo hayo.
Awali, matokeo hayo ya kura za maoni yaliahirishwa kutangazwa kutokana na kuwepo kwa tuhuma za kuwapo kwa wizi wa kura. Kwa jimbo la Tarime Mjini, Lugola alifafanua kuwa Michael Kembaki ndiye aliyeibuka mshindi kwa kura 3,908 akifuatiwa na Kabaka aliyepata kura 2,411.
Katika Jimbo la Tarime Vijijini, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Christopher Kangoye ambaye amejaribu zaidi ya mara tatu kuusaka ubunge, lakini bila mafanikio aliibuka mshindi akivuna kura 15,928 dhidi ya 12,205 za John Gimunta ambaye ni Mweka Hazina wa CCM wilayani Tarime.
Nyangwine na Gimunta, baadaye walilalamikia matokeo hayo wakisema mchakato wa kura za maoni ulitawaliwa na hujuma.
Kayombo azidiwa Mbinga Katika Jimbo la Mbinga Vijijini, matokeo yaliyotangazwa saa 5:45 usiku baada ya mvutano wa kutangaza matokeo unaodaiwa kudumu kwa takribani saa 12, yameonesha kuwa mbunge wa jimbo hilo aliyekuwa amejitokeza kutetea kiti chake, Gaudence Kayombo ameshindwa katika kura za maoni ndani ya CCM.
Aliyeibuka mshindi ni Martin Msuha, aliyepata kura 13,354 dhidi ya 12,068 za Kayombo, ambaye pia kwa mwaka mmoja na nusu kati ya Januari 12, 2007 na Agosti 2, 2008 alikuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.
Wengine walioshiriki katika mchakato wa ubunge jimboni humo na kura zao kwenye mabano ni Humphrey Kisika (545), Dk Silverius Komba (1,289), Edesius Kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga (3,941) na Deodatus Ndunguru.
Wabunge Singida hoi MCHUANO wa makada mbalimbali wa CCM kuwania nafasi za ubunge katika mkoa wa Singida umekamilika, huku wabunge waliokuwa wakitetea nafasi zao na baadhi ya vigogo kwenye chama hicho wakiwa wamebwaga vibaya.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Singida, Mary Maziku, wabunge wawili waliokuwa wakitetea nafasi zao hawakuweza kupata kura za kutosha kwenye kura za maoni. Nao ni Salome Mwambu wa Jimbo la Mkalama na John Lwanji wa Manyoni Magharibi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai ambaye aligombea jimbo la Mkalama alifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye kinyang'anyiro hicho kwa kupata kura 3,908 nyuma ya Allan Kiula aliyezoa kura 5,823. Jimbo hilo lilikuwa na wagombea 16.