Thursday, August 13, 2015

Wafanyakazi Daraja la Kigamboni wagoma.




Wafanyakazi Daraja la Kigamboni wagoma.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Wafanyakazi wa Kampuni ya China Major Bridge Engineering Co. ltd wamegoma kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigamboni, wakiushinikiza uongozi kuwalipa madai yao.  Miongoni mwa mambo wanayodai ni malipo ya mshahara wa kima cha chini cha Sh. 325,000 kilichotangazwa na serikali pamoja na  kuwapatia mikabata ya kazi.  

Khamis Mpili, alisema tangu mradi wa ujenzi huo uanze kuna wafanyakazi hawajapatiwa mikataba ya kazi, hali inayosababisha kukosa haki zao za  msingi zikiwamo malipo ya likizo, nyongeza ya mishahara, na kuingiziwa fedha za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (Nssf).

"Kuna wafanyakazi wana mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu hawana mikataba ya kazi, tunataka uongozi utupatie stahiki zetu tuendelee na kazi," alisema Mpili.

Aidha, alisema wanafanya kazi kwa saa 84 badala ya saa 45 bila kupewa likizo na kwamba baadhi ya wafanyakazi walipata ulemavu cha kushangaza wameachwa bila kupatiwa matibabu kufuatana na sheria za ajira zinavyoelekeza. 

Alisema viongozi wa NSSF walikwenda eneo la ujenzi na kuwaandikisha wafanyakazi wachache katika fomu za usajili huku wengine wakikosa fomu hizo.

Alidai kuwa waliowateua kuwapigania haki zao walifukuzwa kazi na uongozi.

Izua Sosthenes, alisema Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka (pichani), alifika  ofisi za makandarasi hao, lakini hakuonana na wafanyakazi wamueleze matatizo yao.
Alisema, siku nyingi zimepita tangu, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, alipokwenda kukagua ujenzi wa daraja hilo.

Mhandisi wa kampuni hiyo, Liu Tao, alisema kampuni yao iliingia mkataba na serikali mwaka 2012 kabla ya sheria ya mshahara wa kima cha chini haijabadilishwa. 

Alisema watafanya juu chini kuhakikisha  wanaanza kuwalipa baadhi ya wafanyakazi madai yao na kuahidi wengine watamaliziwa haraka iwezekanavyo.

Aliongeza kuwa baada ya kuwalipa, ujenzi utaendelea na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Mwanasheria wa Wizara ya Kazi na Ajira, Omari Sama, alisema walichokigundua ni uelewa mdogo wa matakwa ya sheria za kazi kati ya mwajiri na waajiriwa, hivyo walichofanya kutoa elimu kwa pande zote mbili.

Meneja Mradi huo kutoka NSSF, Karim Mattaka, alisema mgomo walioufanya wafanyakazi  wa kampuni ni batili kwa kuwa wamekwenda kinyume cha sheria cha kufanya migomo zinavyoeleza.

Alisema jana hakukutakiwa kufanyika mgomo bali ilikuwa siku ya kulipwa madai yao kwa kuwa Mwanasheria Sama alishawapa taratibu zote za kufanya mgomo.