Wednesday, August 12, 2015

Sasa niko fiti, asema Mbowe


Sasa niko fiti, asema Mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Dk. Shem Sanga, alisema alisumbuliwa na uchovu

Afya ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Taifa ya Muhimbili, Kitengo cha Moyo imeimarika na leo ataruhusiwa.
 
Daktari bingwa wa moyo katika hospitali hiyo, Dk. Shem Sanga, alisema baada ya Mbowe kupokelewa juzi na kufanyiwa vipimo, alibainika kusumbuliwa na tatizo la uchovu wa mwili uliosababishwa na kufanya kazi mfululizo bila kupumzika pamoja na kutopata chakula cha kutosha.
 
Dk. Sanga alisema Mbowe alifikishwa katika hospitali hiyo juzi akitokea hospitali ya Doktors Plaza iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam na mpaka jana alikuwa ameangaliwa na madaktari bingwa wanane
Tatizo hilo la uchovu lilimkuta Mbowe wakati akitokea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), alikokuwa amemsindikiza mgombea wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, kuchukua fomu.
 
Juzi Lowassa alichukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusindikizwa na viongozi wa vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi, NLD, Chadema pamoja na wafuasi wao.
 
Kutokana na watu wengi kujitokeza kumsindikiza Lowassa kuchukua fomu juzi shughuli mbalimbali za wananchi zilisimama huku barabara kadhaa jijini Dar es Salaam zikifungwa kwa muda kupisha msafara.
 
Akizungumza katika hospitali hiyo jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema afya ya Mbowe iko vizuri na kuwataka Watanzania kuendelea kuwaombea viongozi wa Ukawa katika kipindi hiki kigumu kuelekea uchaguzi mkuu. Mbowe akizungumza jana alisema, anajisikia vizuri na kuwapongeza madaktari wote waliompokea na kumpatia huduma. Alisema juzi akiwa njiani kutokea Nec alijikisikia kizunguzungu na kuomba apelekwe hospitali kwa ajili ya kuangalia hali hiyo inatokana na kitu gani.
 
Aliwaambia waandishi wa habari kwamba baada ya kufika Muhimbili na kufanyiwa vipimo madaktari walimwambia kwamba kizunguzungu alichopata kilitokana na uchovu uliotokana na kufanya kazi mfululizo bila kupumzika na kutopata chakula cha kutosha.
 
"Niko salama, wananchi msiwe na wasiwasi, nilifika hapa nikapokelewa vizuri na kupewa mapumziko ya saa 48 na niwaombe radhi wapenzi ambao wanazuiwa kuja kuniona kutokana na utaratibu ulivyo hapa hospitali," alisema Mbowe. Mbowe akizungumza huku amezungukwa na madaktari katika ukumbi wa mikutano hospitalini hapo, alisema akishapumzika kwa huo muda wa saa 48 aliopewa atatoka ili kuendelea na shughuli za kuelekea uchaguzi mkuu.