Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kura za maoni za kuwapata wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa ubunge na uwakilishi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu zimetawaliwa na vitendo vya rushwa.
Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (Zaeca), imewakamata makada kadhaa wa chama hicho, wakituhumiwa kugawa rushwa ya fedha, nguo na wengine kuunganishwa umeme kwenye nyumba zao.
Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE, Mkurugenzi wa Zaeca, Mussa Haji Ali, alisema makada wengi wakiwamo vigogo wa chama hicho wanatuhumiwa kutoa rushwa katika mchakato huo.
Alisema maofisa wake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliwakuta wanasiasa hao kwenye maeneo mbalimbali wakitoa rushwa kwa wana-CCM na viongozi wa matawi wa chama hicho.
Alisema kuwa miongoni mwa vitu walivyokutwa wakigawa wakiwa kwenye kampeni ni fedha taslimu, kanga na kofia.
Alisema uchunguzi dhidi ya makada hao ukikamilika, watawasilisha majalada ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya kufungua mashitaka.
Alisema wanao ushahidi wa kunaswa na vipaza sauti, wa picha za mnato na picha za video.
Mmoja wa watuhumiwa ni aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Magomeni.
Alisema mgombea huyo alitiwa nguvuni nyumbani kwake wakati akiwagawia kofia watu 40, doti za kanga na fedha taslimu kwa makatibu wa matawi wa chama hicho.
Mkurugenzi huyo wa Zaeca, alisema wamewakamata watu waliojitambulisha kuwa ni wapambe wa aliyekuwa miongoni mwa wagombea wa Jimbo la Paje kwa nafasi ya uwakilishi na ubunge kati ya hao akiwa na Sh. 850,000 na doti 100 za kanga.
Taasisi hiyo pia ilimkamata mgombea ubunge mmoja wa jimbo la Chwaka, akigawa Sh. 5,000 kwa kila mwanachama.
Alisema katika maeneo ya Kibirikani Fuoni alikutwa mgombea uwakilishi akigawa fedha, lakini baada ya kupata taarifa kuwa Zaeca wameizunguka nyumba hiyo, alichoma moto gari aina ya PRADO na kukimbia.
Wengine ni mgombea ubunge wa Jimbo la Magomeni, ambaye alitoa fedha katika akaunti yake na kumtumia mtu kuwagawia wapiga kura huku mgombea mwengine wa jimbo hilo kwa nafasi hiyo hiyo akidaiwa kutoa fedha Benki ya CRDB na kuwatumia wanachama kupitia simu.
Katika jimbo la Amani, mamlaka hiyo ilimkamata mgombea uwakilishi akigawa mchele.
Mamlaka hiyo pia imemnasa mgombea wa ubunge Jimbo la Mpendae, akigawa jezi na mipira kwa timu mbili za soka na Sh. 250,000 huku akikusanya mabalozi wa zoni tatu na kuwapa Sh. 5,000. Anadaiwa kuwagawia viongozi wa matawi Sh. 10,000 kila mmoja.
Pia anadaiwa kuwakusanya watu wasiopungua 40 katika Chuo cha Msolopa Kilimani na kuwapa Sh. 5,000 kila mmoja.
Katika Jimbo la Malindi, Zaeca ilimkamata mgombea ubunge akigawa Sh. 5,000 na watu watatu ambao baada ya kuhojiwa walikiri kuzipokea.
Alisema katika Jimbo la Kikwajuni walimnasa mgombea ubunge katika eneo la Michezani na Sh. milioni 10 akiwa amewakusanya makatibu wa CCM jimbo na wasimamizi wa uchaguzi ili kuwagawia fedha hizo.
Kwa mujibu wa Ali, mgombea uwakilishi mmoja alikutwa akivikusanya vikundi vya kinamama kwa kutoa Sh. 5,000 kwa kila mmoja katika maeneo ya Muembe Ladu.
Yumo pia mmoja wa wagombea ubunge wa Jimbo la Chumbuni aliyekutwa akivikusanya vikundi 10 katika tawi la CCM na kukipatia kila kimoja Sh. 150,000.
Ali aliongeza kuwa mmoja wagombea uwakilishi jimbo la Mfenesini, alikutwa akiwa na mkewe maeneo ya Mwakaje wakitoa fedha na kwamba baada ya kuwaona watendaji wa Zaeca, mkewe alikimbia huku dereva akikutwa na Sh. 500,000.
Katika jimbo la Tumbatu, mgombea wa ubunge alikamatwa akidaiwa kusambaza nguzo za umeme na kuwaunganishia umeme wakazi wa kijiji cha Tumbatu kwa gharama zake.
Katika Jimbo la Donge mmoja wa wagombea ubunge alitumia wapambe wake kuwapa wapiga kura fedha.
Kwa upande wa viti maalum vya ubunge na uwakilishi, taasi hiyo pia iliwatia mbaroni wagombea watatu wa ubunge na watatu wa uwakilishi wanaodaiwa kuwakusanya wakazi 30 wa maeneo ya Pangawe na Kijitoupele na kuwapa Sh. 100,000 kila mmoja.
CHANZO: NIPASHE