Friday, July 24, 2015

TANESCO KUANZA KUTUMIA NGUZO ZA ZEGE




TANESCO KUANZA KUTUMIA NGUZO ZA ZEGE

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lipo katika mchakato wa mwisho wa kuanzisha kampuni ya kutengeneza nguzo za umeme za zege, ikiwa ni mkakati wa uboreshaji huduma kwa wateja wake, kupunguza matumizi ya nguzo za miti na kudhibiti uharibifu wa miundombinu hiyo.


 
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba (pichani), alisema kampuni hiyo ambayo itakuwa chini ya shirika hilo inatarajiwa kuanza kazi mwishoni mwa mwaka huu mchakato wa kuisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  (Brela) utakapo kamilika.
 
Alisema hatua ya shirika hilo kuanza kutumia nguzo za zege badala ya za miti ni moja ya mikakati ya shirika ilo kuhakikisha linatoa huduma bora na za uhakika kwa wateja wake kwani mara nyingi nguzo za miti zimekuwa hazidumu na kulazimika kubadilishwa mara kwa mara kutokana na uchakavu.
 
"Teknolojia inakuwa kila siku na kurahisisha huduma kwa wananchi na hata wakati mwingine kupunguza gharama, tutakapoanza kuzalisha nguzo za zege tutapunguza kero nyingi kwa wateja wetu kwani nguzo za miti huharibika haraka hasa kipindi cha mvua pamoja nyingine kuungua moto unapotokea," alisema.
 Mramba alisema kutumika kwa nguzo hizo za zege pia kutabadilisha mandhali ya miji na kuongeza kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.
 
Kuhusu uboreshaji wa huduma ya umeme kwa jiji la Dar es Salaam, Mramba alisema ujenzi wa vituo vidogo vitano vya usambazaji na upozaji wa umeme unaendelea vizuri pamoja na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika eneo la Mbagala na Vijibweni na kusababisha kazi hiyo kuchelewa kukamilika.
 
Alisema vituo hivyo vilitakiwa kuwa tayari mwezi ujao lakini kutokana na changamoto hizo sasa vitakamilika mwishoni mwa  mwaka huu na kwamba kituo cha Kinyelezi na City Centre  vinategemewa kukamilika  Agosti, mwaka huu.