Arumeru. "Ingawa haikuhitajika ushahidi wa kimahakama, mchakato wa uteuzi wa mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki mwaka 2012, uligubikwa na tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa makusudi wa kanuni za chama kwa lengo la kuwabeba baadhi ya wagombea."
Hiyo ni kauli ya kada wa CCM, William Sarakikya anayeomba kuteuliwa kugombea ubunge Arumeru Mashariki. Alisema hayo alipotakiwa kueleza kwa nini anadhani anaweza kushinda ubunge safari hii, wakati alishindwa katika uchaguzi mdogo wa mwaka 2012.
Mbali na Sarakikya wengine wanaoomba kuteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo ni Elirehema Kaaya, Sioyi Sumari, John Pallagyo, Angela Pallagyo na Daniel Pallagyo.
Sarakikya alisema uchaguzi mdogo uliofanyika kujaza pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Jeremiah Sumari, ulishuhudia matumizi makubwa ya fedha kiasi cha kuibua usemi wa 'kula CCM, kura Chadema'.
"Baadhi ya viongozi na makada wa CCM walidaiwa kukisaidia Chadema baada ya kuchukizwa na jinsi CCM ilivyoendesha uteuzi ambao ulirudiwa mara mbili kutokana na matokeo ya awali kubatilishwa na vikao vya juu," alisema.
Katika uchaguzi huo mdogo, Sarakikya aliibuka mshindi wa pili nyuma ya Sioyi Sumari, ambaye hata hivyo alishindwa kwa zaidi ya kura 6,000 na mgombea wa Chadema, Joshua Nassari.
Vipaumbele vyake
"Nikifanikiwa, jukumu langu la kwanza ni kuwaunganisha Wanaarumeru bila kujali tofauti zao kiitikadi. Hii itatusaidia kushirikiana katika shughuli za maendeleo kwa sababu maendeleo hayana itikadi," alisema Sarakikya.
Anataja kipaumbele kingine kuwa ni kushughulikia tatizo la miundombinu ya barabara na kusaidiana na wakazi wa jimbo hilo kutafuta njia mbadala ya kipato, baada ya zao la kahawa lililokuwa likitegemewa kushuka bei katika soko la kimataifa.
Uhaba wa majisafi na salama ni changamoto ya nne ambayo Sarakikya alisema ataivalia njuga kuitatua kwa kuchimba visima virefu vya maji katika kila kijiji chenye chanzo cha maji.
Sarakikya ambaye hata akishinda kura ya maoni ya CCM, atalazimika kukabiliana na ushindani mkali kutoka kwa mbunge wa sasa aliyepita bila kupingwa ndani ya chama chake Chadema, Joshua Nassari, alitaja suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi kama changamoto ya tano atakayoitafutia ufumbuzi.
"Nitaanzisha programu maalumu itakayounganisha wananchi na vyuo vikuu vitatu vilivyoko Arumeru; Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Arusha na Tumaini Makumira ili kuwawezesha wananchi kunufaika na tatifi za kisomi za kijamii na kisayansi zinazofanywa na wakufunzi na wanachuo hao," alisema.
Suala la afya ya msingi kwa kila mwananchi ni jambo la sita analolitaja katika vipaumbele vyake. Alisema anakusudia kuhamasisha kila kaya kujiwekea bima ya afya itakayowahakikishia wananchi tiba sahihi na nafuu kila wanapohitaji huduma za kitabibu.
"Nitahakikisha wazee, akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanapata huduma bora na stahiki za afya kama sera ya afya inavyoelekeza tofauti na sasa na makundi haya aidha wanalipishwa gharama au wanapewa huduma hafifu," anasema.
Kuhusu ardhi Sarakikya alisema: "Ardhi ni kati ya masuala nyeti Meru kabla na baada ya uhuru. Lazima wananchi na wawekezaji wafikie makubaliano ya hiari na yenye maridhiano yatakayonufaisha pande zote mbili.
Alisema atatumia nafasi yake ya ubunge kuishawishi Serikali ili itekeleze uamuzi wa kufuta hati za mashamba yote yasiyoendelezwa kwa muda mrefu na kuyagawa kwa wananchi.