Wednesday, July 29, 2015

NEC yaongeza saa uandikishaji BVR Dar kutoka saa moja asubuhi badala ya saa mbili ya sasa hadi saa 12 jioni



NEC yaongeza saa uandikishaji BVR Dar kutoka saa moja asubuhi badala ya saa mbili ya sasa hadi saa 12 jioni
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeongeza saa za kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) mkoani Dar es Salaam kutoka saa moja asubuhi badala ya saa mbili ya sasa hadi saa 12 jioni.Tume imesema hatua hiyo imefuatia malalamiko ya wakazi wa mkoa huo kuwa baadhi ya vituo vinachelewa kufunguliwa na kufungwa mapema.
 
Kadhalika NEC imesema idadi ya waliokwishaandikishwa kwenye daftari hilo hadi juzi jijini humo, imefika 1,172, 855 kwa Kinondoni watu 490,228, Temeke 389,558 na Ilala 302, 871.
 
Pia jumla ya mashine za BVR ambazo hadi sasa zitatumika katika uandikishaji katika jiji hilo ambalo ni mkoa wa mwisho katika kazi hiyo ni 3,717 kwa Ilala yenye vituo 395, ina BVR 927 sawa na asilimia 117, Kinondoni yenye vituo 702, BVR 1462 sawa na asilimia 104 huku Temeke yenye vituo 572 ikiwa na BVR 1,328 sawa na asilimia 116.
 
Hata hivyo, NEC imesema mashine hizo zinatarajiwa kuongezwa kadri ya uhitaji wake kwenye vituo vya kujiandikisha.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, baada ya kukutana na uongozi mzima wa Mkoa wa Dar es Salaam kujadili uandikishaji huo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva (pichani), alisema vituo vya kujiandikisha vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa mbili hadi saa 12 jioni.
 
Alisema kwa sasa tume hiyo haiwezi kuzungumza iwapo imeongeza muda, lakini itahakikisha watu wote waneandikishwa mkoani humo.
 
Jaji Lubuva aliongeza kuwa maofisa uandikishaji wote wasio na uzoefu wa kutosha kwenye vituo wataondolewa na kutaka makundi maalumu wakiwamo wazee, wajawazito wapewe kipaumbele.