Saturday, June 06, 2015

NITAONGOZA NCHI KISAYANSI-DK: BILAL



NITAONGOZA NCHI KISAYANSI-DK: BILAL
Dodoma. Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amesema nchi inaendelea kupoteza maadili, hivyo kuahidi kusimamia uwajibikaji katika sekta ya umma endapo atapitishwa na CCM na kisha kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu ya kuomba kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo, Dk Bilal alisema Serikali yake haitavumilia uvunjwaji wa miiko ya uongozi.
Huku akisisitiza kuwa kaulimbiu yake, ni mabadiliko ndani ya umoja, Dk Bilal alisema vipaumbele vyake ni kusimamia matumizi mazuri ya rasilimali za Taifa na kuboresha na kusimamia matumizi ya mapato. Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kulinda haki za binadamu na kuhakikisha nchi inasimamiwa kwa misingi ya sheria.
"Nitahakikisha Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea, kusimamia na kuimarisha utawala wa sheria, haki za binadamu, haki za kina mama na watoto, walemavu hasa wa ngozi, haki ya kuunda na pamoja na uhuru wa kupata habari."
Dk Bilal alisema atahakikisha analinda misingi ya utaifa ulioasisiwa na wazee na ambayo imelifikisha Taifa katika miaka 54 likiwa moja, imara, lenye upendo na mshikamano.
Alipotakiwa kuwatoa hofu watu wanaodhani kuwa ana mitazamo ya kihafidhina, Dk Bilal alisema yeye ni mwanasayansi na siku zote sayansi inabadilika kulingana na mazingira.
"Hakuna uamuzi uliokuwa sahihi zaidi ya uamuzi wa kisayansi. Mimi siku zote uamuzi wangu unafuata utaratibu huo, ndivyo nilivyolelewa na kufunzwa na nitaendelea kuongozwa kisayansi," alisema.
Akijibu swali lililomtaka afafanue mtazamo wa watu kwamba sasa ni zamu ya Zanzibar kutoa Rais, Dk Bilal alisema chama chake hakina vitu hivyo, bali kinachagua kiongozi au mwanachama ambaye ataweza kuwavusha.
"Hatujali wapi ametoka, hatujali rangi yake, hatujali kabila lake, hatujali dini yake ilimradi ni Mtanzania. Mimi ninadhani ninaweza kulivusha Taifa hili," alisema.
Alisema amejitokeza kwa sababu anayo hamu na uwezo wa kulifikisha Taifa liwe la kutiliwa mfano.
Alisema Muungano ulivyo hivi sasa si kama hapo zamani, sasa unakabiliwa na changamoto nyingi zaidi kwa hiyo ni jukumu lake kuhakikisha kuwa anashirikiana na wadau mbalimbali ili kutatua changamoto zilizopo.
Hali ilivyokuwa
Kabla ya kuingia ndani ya ukumbi, wakati na baada ya kuzungumzia na waandishi wa habari, Dk Bilal alikuwa akishangiliwa na wapambe wake kila mara alipojibu swali la mwandishi au kumaliza hatua moja kwenda nyingine.
Mbali na kushangiliwa wakati anaingia baadhi ya wapambe walijipanga nje ya mlango wa kuingilia jengo la makao makuu kwa ajili ya kumlaki.
Alisindikizwa kwa nyimbo za hamasa za CCM na za kumpongeza. Wapambe hao na baadhi ya watumishi wa ofisi za makao makuu ya chama walikuwa wamevalia mavazi yenye rangi za chama.
Baadhi ya nyimbo zilizosindikizwa na makofi ni pamoja 'Dk Bilal tutamlinda na kumtetea'.
Dk Bilal ni nani?
Alizaliwa Februari 9, 1945 na kuhitimu Shule ya Msingi Makunduchi mwaka 1958. Aliendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Beit-el-Ras mwaka 1962 na baadaye Lumumba zote za visiwani Zanzibar.
Kabla ya kuhitimu kidato cha tano, alipata ufadhili wa kwenda kusoma Marekani katika Chuo Kikuu cha Howard na kuhitimu Shahada ya Fizikia na Hesabu mwaka 1967.
Dk Bilal aliendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Fizikia na kuhitimu mwaka 1969, kisha alianza kufanya kazi akiwa mhadhiri msaidizi na baadaye kuwa mtafiti msaidizi katika Kampasi ya Berkely katika Chuo Kikuu cha Carlifonia.
Mwaka 1976, alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD), ya Fizikia chuoni hapo. Baadaye, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akiwa mhadhiri na mwaka 1983 alipandishwa cheo hadi kuwa Mkuu wa Idara ya Fizikia ya Nyuklia.
Dk Bilal alishiriki katika ukuzaji wa sekta ya nyuklia nchini kwa kuwa mmoja wa walioanzisha taasisi ya Serikali inayoshughulikia masuala ya mionzi na mwaka 1988 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sayansi cha UDSM.
Mwaka 1990 alipandishwa cheo na kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu. Safari ya kisiasa ya kada huyo wa CCM ilianza mwaka 1995 alipoteuliwa kuwa Waziri Kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi mwaka 2,000 aliporithiwa na Shamsi Vuai Nahodha.
Mwaka 2010, mwanasayansi huyo aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Makamu wake baada ya Ali Mohammed Shein kuchaguliwa kuwa Rais wa SMZ.