Wafanyikazi wa mashirika ya kutoa misaada wamesema kuwa tetemeko la hapo jana nchini Nepal limeathiri kwa kiasi kikubwa
juhudi za kutoa misaada kwa waathiriwa wa tetemeko la awali lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 8000 takriban majuma mawili yaliyopita.
Mashirika ya misaada yanasema kuwa maporomoko mapya ya ardhi sasa yemekatiza usafiri baada ya kuziba mabarabara yaliyokuwa yamesazwa na tetemeko la awali.
Hadi kufikia sasa inakisiwa kuwa takriban watu 65 wamepoteza maisha yao nchini Nepal huko maafa zaidi yakitarajiwa nchini India na Tibet ,China.
Shughuli za uokozi zimerejelewa Nepal, ambayo kwa mara ya pili ndani ya wiki tatu imekumbwa na tetemeko kubwa la ardhi.
Lakini bado kuna watu waliozikwa kwenye vifusi.
Maafisa wa huko wanasema kuwa wanatarajia idadi hiyo kuongezeka.
Kufikia sasa takriban watu 1,000 wamejeruhiwa na tetemeko hilo lipya.
Waathiriwa wengi wameripotiwa kufunikwa na vifusi karibu na kitovu cha tetemeko hilo katika mji wa Chautara
Watu wengi wamelala nje wakihofia kuwa wanaweza kuathirika zaidi wakiwa ndani ya nyumba zao.
Wakati huo huo helikopta ya kikosi cha majini cha Marekani,ambayo ilikuwa ikifanya kazi ya kusaidia kusambaza huduma za kibinaadamu nchini Nepal, haijulikani iliko.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa, ndani ya helikopta hiyo kulikuwa na watu wanane,miongoni mwao, sita ni askari wa kikosi cha majini cha Marekani na askari wawili wa jeshi la Nepal.
Maofisa wa serikali wa Marekani wamesema kwamba helikopta hiyo ilikuwa maeneo ya jirani na kijiji cha Charikot, ambacho kiliharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi.