Serikali itatumia zaidi ya Dola milioni 300 sawa Shilingi bilioni 600 kuboresha Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kujenga mifereji mikubwa ya kubeba maji ya mvua ili kukabiliana na mafuriko.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), Hawa Ghasia (pichani), alitangaza jana bungeni wakati akitoa maelezo ya mapitio ya kazi kwa mwaka 2014/15 na mwelekeo wa mwaka 2015/16.
Alisema mpango huo unaoitwa Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP) utaimarisha miundombinu ya kudhibiti mafuriko kwa kujenga mifereji mikubwa na midogo ya maji ya mvua katika maeneo yenye mafuriko yakiwamo ya mabondeni na mitaani iliyojengwa bila mipango.
Kadhalika, Ghasia alisema DMDP itajenga barabara za mitaa za kuunganisha Jiji na mtandao wa mabasi yaendayo haraka (DART).
"Pamoja na kuboresha na kuimarisha mfumo wa ukarabati wa miundombinu utahusika na mpango wakuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuimarisha matumizi bora ya ardhi…" alisema.
Hatua ya serikali inatangazwa, baada ya miaka mingi ya mafuriko jijini na ni wiki iliyopita watu zaidi ya nane walipoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyotokea mabondeni na sehemu zilizojengwa bila kuzingatia taratibu za mipango miji.
Akingumzia elimu, alisema usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza umeshuka mwaka huu wa fedha ikilinganishwa na miaka ya nyuma, chanzo kikiwa ni pamoja na utumikashwaji watoto kwenye ajira.
"Uwiano umepungua kwa asilimia 2.9 kutoka asilimia 96.2 mwaka 2013 na kufikia 93.3 mwaka jana . Kupungua kumetokana na sababu kadhaa kama utumikishwaji, kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, mwamko duni wa wazazi na walezi kuhusu elimu." Aliongeza.
Aidha alizungumzia mafanikio ya elimu kwamba idadi ya shule za sekondari za kidato cha tano zimeongezeka kutoka 179 (2010) hadi 245 mwaka huu.
Kuhusu barabara, alisema zimejengwa 4,234 kufikia Machi mwaka huu, wakati nyingine 5,979 zinaendelea kujengwa . Kwa ujumla zinahitajika maabara 10,389.