WAKATI Tanzania ikiwa imeshindwa kutekeleza Malengo ya Milenia wadau wa uchumi wametoa mbinu za kujikimu katika bajeti badala ya kutegemea nchi wahisani.
Malengo manane ya Milenia ni pamoja na suala la kuondoa umasikini na njaa, elimu ya msingi kwa wote, usawa wa jinsia, kuzuia vifo vya watoto, afya ya uzazi, kupambana na Ukimwi, malaria na magonjwa mengineyo.
Akizungumza katika mkutano kuhusu Malengo ya Milenia, Dar es Salaam jana, Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dk. Oswald Mashindano alisema miongoni mwa sababu za kutotekelezeka kwa malengo ya milennia ni ufinyu wa bajeti.
"Sababu kubwa ya kukosekana kwa rasilimali fedha ni tabia ya wafadhili kutotekeleza ahadi zao hasa asilimia 07 ya msaada wa maendeleo kwa nchi zinazoendelea (ODA)," alisema Dk. Mashindano.
Alisema badala ya kuendelekeza nchi wafadhili, Serikali inapaswa kuwa na vyanzo vingine ikiwa pamoja na vyanzo vya ndani.
"Kunatakiwa kuwe na chanzo kikuu cha fedha za maendeleo kama inavyoelezwa kwenye sera za taifa na mikakati ya maendeleo. Tuimarishe ushiriki wa sekta binafsi katika mikakati ya maendeleo katika ngazi za wilaya kama vile mipango ya wilaya na mipango ya uchumi na jamii," alisema.
Alishauri pia kuimarishwa kwa mfumo wa kodi nchini kwa kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato hadi kwenye sekta zisizo rasmi.
"Kupambana na utoroshwaji wa fedha haramu nje ya nchi, ukwepaji wa kodi na rushwa, itasaidia. Inatakiwa pia kuongeza uwazi na kuhakikisha malipo yote ya Serikali yanakuwa wazi," alisema.
"Tunatakiwa pia kuongeza faida kutoka katika sekta ya uchakataji kwa kutekeleza Mkakati wa Uwazi katika Sekta ya Uchakataji (EITI),"alisema
Awali akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Kuondoa Umasikini katika Wizara ya Fedha, Anna Mwasha alikiri Serikali kushindwa kutekeleza malengo yote ya millenia kwa kipindi cha miaka 15, akisema mikakati zaidi inafanyika.
"Wengi wetu tunatambua matokeo ya miaka 15 ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia tumeshindwa kutekeleza katika baadhi ya maeneo na inajulikana kama 'biashara iliyoshindikana'," alisema Mwasha.