Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amerejea nchini humo, huku naibu kiongozi wa mapinduzi akikiri kuwa jaribio la kumuangusha Nkurunziza limeshindwa. Umoja wa Mataifa umetaka kurejeshwa haraka utawala wa sheria.
Mshauri mwandamizi wa mawasiliano wa rais Willy Nyamwitwe, alisema Nkurunziza amerejea nchini humo, lakini hakutoa maelezo zaidi kwa kile alichosema ni sababu za kiusalama.
Nkurunziza alikuwa nchi jirani ya Tanzania kwa ajili ya mazungumzo ya kikanda siku ya Jumatano wakati mapinduzi yalipotangazwa na Jenerali Godefroid Niyombere, na kufunika wiki kadhaa za maandamano dhidi ya jaribio la rais kutafuta muhula wa tatu.
Taarifa za kurejea kwa rais Nkurunziza hazikuweza kuthibitishwa na duru huru hata hivyo, na uwepo wake umeendelea kuwa kitendawili usiku wa Alhamisi.
Lakini tangazo kwamba amerudi lilifuatia haraka na kukiri kwa naibu kiongozi wa mapinduzi Cyrille Ndayirukiye kwamba mapinduzi hayo yameshindwa.
Ndayikuriye aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa binafsi anatambua kuwa vuguvugu lao limeshindwa.
Wanajeshi Watiifu wadhibiti vituo muhimu
Mapema Alhamis, wanajeshi watiifu kwa rais walisema walizuwia mashambulizi mawili makubwa yaliyofanywa na wapinzani katika mapambano makali ya kudhibiti kituo chenye umuhimu wa kimkakati cha redio ya taifa.
Miili ya wanajeshi watatu ilionekana ikiwa imelala mitaani karibu na eneo la mapigano hayo, ishara ya kwanza ya maafa katika kadhia hiyo ya mapinduzi.
Kufikia mchana, mkurugenzi wa kituo hicho Jerome Nkokirantevye alisema wanajeshi watiifu ndiyo walikuwa wanakidhibiti kituo hicho.
Kufikia mchana, mkurugenzi wa kituo hicho Jerome Nkokirantevye alisema wanajeshi watiifu ndiyo walikuwa wanakidhibiti kituo hicho.
Afisa mwanadamizi wa polisi alithibitisha taarifa hizo na kusema jana jioni kuwa wanajeshi wanaounga mkono mapinduzi walisambaratika baada ya mashambulizi yao dhidi ya Televisheni ya taifa RTNB na jengo la redio katika mji mkuu kukandamizwa. Alisema baadhi ya waasi tayari wamejisalimisha na wengine walikimbia.
Tangazo la mapinduzi la Jumatano lilisababisha ukosoaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia, na kuibua hofu ya kurejea katika vurugu kubwa katika taifa hilo maskini, ambalo bado linaendelea kuhisi athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 13 vilivyomalizika mwaka 2006, na kugharimu maisha ya maelfu ya Warundi.
Baraza la Usalama laonya
Marekani ilisisitiza Alhamis kuwa Nkurunziza ndiye rais halali wa Burundi . Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana katika kikao cha dharura siku ya Alhamis, lililaani jaribio hilo la mapinduzi, na kutaka kurejeshwa haraka kwa utawala wa sheria na kufanyika kwa uchaguzi kwa kuzingatia makubaliano ya Arusha.
Katika taarifa iliyosomwa na Raimonda Murmokaite, balozi wa Lithuania katika Umoja wa Umoja wa Mataifa, na rais wa barala hilo kwa mwezi wa Mei, baraza hilo lenye wanachama 15 lilieza utayarifu wake kuchukulia hatua vitendo vya vurugu nchini Burundi vinavyotishia amani na usalama.
"Wanachama wa baraza la usalama wamelaani machafuko nchini Burundi na hasa wamewalaani wanaochochea vurugu za aina yoyote dhidi ya raia, na wale wanaotaka kutwaa madaraka kwa njia zisizohalali," alisema Murmokaite.
"Wanachama wa baraza la usalama wametoa wito kwa pande zote kutotumia vurugu na kutoa kipaumbele kwa amani na usalama. Baraza pia limerejelea uungaji wake mkono wa juhudi la mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Said Djinnit, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki."
Chanzo: DW