Monday, May 11, 2015

NYALANDU: VIONGOZI WAKO BEGA KWA BEGA NA MAJANGILI


NYALANDU: VIONGOZI WAKO BEGA KWA BEGA NA MAJANGILI
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amedai kuwa majangili wote wanaotiwa mbaroni na vikosi vya Askari wa Wanyamapori, wanadaiwa wanatumwa na watu waliopo kwenye ofisi za serikali na wengine nje ya nchi.


Amesema mtandao wao ni mkubwa lakini ameapa kula nao sahani moja. Nyalandu alisema hayo jana wakati wa ziara yake wilayani Masasi mkoani Mtwara, alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Idara ya Wanyamapori, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakuu wa idara na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani hapa.
Sambamba na hilo, amewaagiza maofisa wanyamapori na misitu nchini, kumkamata mwananchi yeyote atakayevamia hifadhi za wanyamapori zilizotengwa.
Nyalandu alisema kuwa hatua ya kwanza ambayo serikali imedhamiria kuchukua katika mapambano hayo dhidi ya ujangili ni kuvipatia vyombo vya ulinzi na usalama vitendea kazi vya kiintelejensia ili vyombo hivyo viweze kufanya kazi kwa kupashana habari kati ya Tanzania na nchi jirani.
Alitaka maofisa wanyamapori na misitu nchini, kufanya kazi zao kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi na kwamba waache kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema ujangili ni tishio kubwa kwa wanyamapori nchini na kwamba kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya sheria na Katiba na Wizara ya Maliasili na Utalii, zimeandaa mpango mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo la ujangili, linaloathiri sekta ya utalii nchini.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama ni nguzo muhimu katika kulinda usalama wa nchi, lakini vyombo hivyo vinaweza kushindwa kutekeleza jukumu hilo, kutokana na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha katika kupashana habari na kupeana taarifa mbalimbali za kiintelejensia.
Nyalandu alisema taifa kila siku linapoteza rasilimali zake muhimu na kwamba jambo hilo linarudisha nyuma uchumi wa taifa, hivyo hatua ya serikali kutaka kuvipatia vyombo vya ulinzi na usalama vitendea kazi vya kisasa, itasaidia kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara ya ujangili nchini.
Kwa mujibu wa waziri huyo, serikali inatambua wajibu na umuhimu wa vyombo vya ulinzi na usalama lakini ili vyombo hivyo viweze kufanya kazi kwa ufanisi, ushirikiano wa karibu ni lazima.
Alisema Wizara ya Maliasili kwa kushirikiana na Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpool) na Idara ya Wanyamapori, watahakikisha wanawasaka majangili wote duniani, lengo likiwa ni kukomesha vitendo hivyo.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobahatika kuwa na idadi kubwa ya wanyamapori, lakini kutokana na vitendo vya ujangili vinavyofanywa na watu wasioitakia mema nchi hii, idadi ya wanyama imeendelea kushuka na kwamba hali hii ikiachwa iendelee ni dhahiri kuwa misitu na mapori, yatabaki wazi bila wanyama.
Awali, akiwasilisha taarifa ya wilaya ya Masasi, Mkuu wa Wilaya hiyo Bernald Nduta alisema Idara ya Wanyamapori wilayani humo, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo upungufu wa watumishi. Waziri alikiri hali hiyo na kuahidi kuleta haraka iwezekanavyo watumishi wawili wa idara hiyo wilayani Masasi.
HABARI LEO