MVUA zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha kutokamilika kwa wakati mradi wa ujenzi wa daraja la kisasa la Kigamboni.
Ujenzi wa daraja hilo linalojengwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa sasa umekamilika kwa asilimia 80.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Meneja wa mradi huo, Karim Mataka, alisema kutokana na hali hiyo wanatarajia kukamilisha ujenzi wa daraja hilo Desemba mwaka huu.
"Pamoja na changamoto zilizotufanya kuchelewa kidogo lakini tunashukuru tunaendelea vizuri na ujenzi huu wa daraja ambalo ni la kisasa na litakuwa na barabara sita," alisema Mataka.
Alisema ujenzi wa daraja hilo unasimamiwa na wahandisi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Wizara ya Ujenzi pamoja na NSSF.