POLISI mkoani Morogoro inamshikilia Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Boniface Jacob (32) , mkazi wa Dar es Salaam kwa kudaiwa kukiuka Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ya Vyama vya Siasa nchini inayozuia uundaji wa vikundi vya ulinzi wa vyama.
Jacob, Diwani wa Kata ya Ubungo, Dar es Salaam kwa tiketi ya chama hicho pia ni Mkufunzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema- Taifa katika kikundi cha ulinzi cha chama hicho maarufu kama `Red Brigade'.
Kukamatwa kwa Jacob kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.
Jacob ambaye anajulikana kwa jina maalumu la K5 alikamatwa kutokana na kudaiwa kukiuka utaratibu wa matumizi ya kibali kilichoombwa na Chadema wilaya cha kufanya mkutano wa hadhara na badala yake ukageuzwa kuwa ni wa kuhitimisha mafunzo maalumu ya ulinzi kwa `Red Brigade'.
Hivyo alisema kiongozi huyo kwa kufanya hivyo amekiuka sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 385 , inayokataza uundaji wa vikundi vya ulinzi kazi ya kuchukua jukumu la Polisi .
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa kuwa vijana hao wamepatiwa mafunzo yenye malengo ya kutumia nguvu za kijeshi licha ya katazo la vyama kuunda na kuwa na vikundi vya aina hiyo.
Walinzi hao waliapishwa baada ya kufanyika gwaride maalumu mbele ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema- Taifa, Wilfred Lwatakare, na kula kiapo cha utii kwa viongozi wa chama hicho.
Akizungumza kabla ya kukamatwa kwake katika tukio la uapishaji wa walinzi hao, Jacob alisema kikosi hicho kina uwezo wa hali ya juu kukabiliana na matukio na ulinzi wa kura pamoja na kikosi cha Poripori ' Kujificha porini'.
Hata hivyo alisema mbele ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama hicho Taifa, kuwa hadi sasa vijana waliofunzwa mafunzo hayo ni 77,000 katika mikoa mbalimbali ya kikanda na lengo la Chama ni kuwa na vijana walinzi 300,000 kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.