Saturday, May 09, 2015

ELIMU YA AFYA YA UZAZI INAEPUSHA WANAFUNZI KUWA NA TAMAA MBAYA



ELIMU YA AFYA YA UZAZI INAEPUSHA WANAFUNZI KUWA NA TAMAA MBAYA
Ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana husababisha mimba katika umri mdogo.

Hii inatokana na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi unatokana na imani potofu miongoni mwa jamii kwamba, kuwapatia elimu hiyo vijana ni sawa na kumruhusu kujihusisha na vitendo vya ngono.
Kutokana na imani hiyo, mimba katika umri mdogo zimekuwa zikiongezeka kwa kasi hivyo kukwamisha maendeleo ya wasichana walio wengi kwa kushindwa kutimiza malengo yao na kuishia kulea watoto bila kuwa na ajira.
Shule katika Wilaya ya Temeke ni miongoni mwa zile zinazokabiliwa na tatizo hilo kutokana na sababu mbalimbali.
"Mahali shule hizo zilipo ni kichocheo tosha cha wanafunzi kupata vishawishi vya kuingia katika mahusiano yasiyokuwa rasmi," anasema Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sophia Mjema.
Anasema wanafunzi hao hupata vishawishi kutoka kwa madereva wa magari ya mizigo yaendayo nje ya nchi kama vile Zimbabwe, Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Kutokana na hali hiyo, Mjema alisema ni lazima kila mwanafunzi ajitambue na kuzingatia kile kilichompeleka shule na kuzishinda changamoto anazokutana nazo.
 "Kwa kufanya hivyo, vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa, wataweza kuepuka vishawishi na hivyo kuwa kichocheo cha maendeleo ya Taifa.
Kufanya vinginevyo, kwa mujibu wa Mjema, watakuwa wanajitengenezea mazingira yasiyo rafiki kwa maendeleo ya kiuchumi kwani itawalazimu kukatisha masomo yao na hivyo kutumia muda mwingi kulea mimba na baadaye mtoto.
"Katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, itakuwa ngumu sana kwa watu wasiokuwa na elimu ya kutosha kuendana na mabadiliko hayo," Mjema anasema.
Anasema ni lazima vijana waandaliwa kwa kufahamu ipasavyo somo la afya ya uzazi vinginevyo atajiingiza katika mazingira yanayoweza kusababisha achanganyikiwe na kujikuta akiokota makopo ili aweze kupata chakula.
Taasisi ya  Wanawake na Maendeleo (Wama), chini ya Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, wameanzisha kampeni ya kutokomeza mimba za utotoni tangu mwaka  2010.
Kampeni hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa njia ya kutoa elimu kwa vijana juu ya afya ya uzazi na stadi za maisha yenye kauli mbiu 'Jilinde utimize ndoto yako'.
Kampeni hii ilianzia mikoa ya Kusini mwa Tanzania mwaka 2010/2012, Mtwara na Lindi vijijini mwaka  2014/2015,  Wama walienda mbali zaidi kwa kuanzisha kampeni hiyo katika Jiji la Dar es Salaam huku Wilaya ya Temeke ikiwa ni miongoni mwa wanufaikaji.
Wama  na  EngenderHealth kwa udhamini wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Msaada la USAID, wamewawezesha vijana 65 na waalimu 11 kutoka shule 11 za wilaya hiyo kupata elimu ya Afya ya Uzazi na stadi za maisha.
Miongoni mwa shule zilizo nufaika na elimu hiyo ni sekondari za Tandika, Temeke, Kibasila, Abdu Jumbe na Mbagala.
Meneja Mawasiliano wa Wama Philomena Marijani anasema Lengo  ni kuwasaidia kuelewa na kupata ujuzi juu ya afya ya uzazi, kuongeza ushawishi na ushiriki wa wazazi, walezi, waalimu na jamii katika kupinga mimba za utotoni.
Marijani anasema mafunzo hayo yatawawezesha Wanafunzi kujiwekea malengo, kufanya uamuzi wa busara, kufikiri kwa makini na kujiepusha na vishawishi rika na mazingira hatarishi
"Tumeanzisha klabu 20 za kijamii zinazojumuisha wazazi, walezi, waandishi wa habari na viongozi wa mitaa zinazosisitiza wote kuwa na wajibu  wa kuleta mabadiliko katika jamii," anasema.
Mabadiliko hayo anasema yana lengo la kuelimisha jamii madhara ya mimba za utotoni.
Ofisa elimu Wilaya ya Temeke, Donaldi Siliva anawataka vijana kuwa na majibu ya kujiamini pale wanapokutana na vishawishi ili kuwakatisha tamaa wale wanaowarubuni.
Wanafunzi hao wameeleza jinsi walivyonufaika na mafunzo hayo kwa kile wanachoeleza ni kujitambua na kuelewa kuwa wanatakiwa kupata elimu ya afya  ya uzazi wakiwa bado hawajabalehe ili watakapofikia wakati huo, wawe wamejiandaa.
Danieli Izack ni mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Tandika, yeye anasema kabla ya kupata elimu, mtaani walikuwa wakidanganyana kujwa matumizi ya uzazi wa mpango yana madhara.
"kupitia elimu tuliopewa sasa naweza kutimiza malengo yangu kwa sababu najua njia ya kuepuka vishawishi," anasema  Izack
Mwanafunzi kutoka Sekondari ya Temeke, Sabrina Baluwani anasema mafunzo hayo yamewanufaisha sana kwani mwanzo walikuwa hawajui ni jinsi gani ya kuepukana na vishawishi rika.
"Tunaenda kuwa waalimu wa wenzetu ambao hawajapata elimu hii, tukiwa shuleni tutaanzisha klabu ambazo tutakuwa tunajadili jinsi ya kuepuka mimba za utotoni, afya ya uzazi na kuepuka maambukizi yatokanayo na zinaa," anasema Baluwani.

Tamko la watoto hao linaashiria kuwa elimu ya uzazi ni muhimu katika shule zote; yaani msingi na sekondari.